Mabasi yote sasa kusimamishwa Morogoro,
Na Andrew Chimesela, Morogoro
Mkoa wa Morogoro umeazimia kusimamisha magari yote yanayopita ndania ya Mkoa huo yakiwemo magari ya abiria na kuwapima abiria waliomo ndani ya vyombo hivyo ili kujua kama wana maambukizi ya virusi vya COVID – 19 ikiwa ni njia mojawapo ya kudhibiti ugonjwa wa CORONA ambao unaonekana kuenea kwa kasi hapa nchini.
Agizo hilo lilitolewa Aprili 21 mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare kwenye kikao cha Wadau mbalimbali wa Mkoa huo kilichoitishwa na Mkuu huyo wa Mkoa na kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Ualimu cha Morogoro kikiwa na lengo la kuweka mikakati ya namna ya kukabiliana na ugonjwa wa CORONA.
Akiwa Mwenyekiti wa Kikao hicho, Loata Sanare amesema hatua hiyo hailengi kuwazuia wasafiri hao kuingia au kupita Morogoro bali inalenga kujua Afya zao katika kujikinga na virusi vya COVID – 19 na kuwakinga wengine hususani wananchi wa Mkoa wa Morogoro hatua ambayo itasaidia kudhibiti ugonjwa wa CORONA usienee kwa kasi ndania ya Mkoa huo na Taifa la Tanzania kwa ujumla.
“tumetembelea jana maeneo mbalimbali ikiwepo Mikese, tuna kituo kule tunaweza tukatumia kuwapima madereva wote wanaokuja, tunavyo vifaa vya kuwapima joto, sio kuwazuia lakini tujue usalama wao” alisema Loata Sanare. “hatukuweza kuwakontroo watu wanaoingia kwenye mji wetu mtatusaidia sasa utatratibu mzuri wa kitaalam wa kuhakikisha watu wanaopita, na watu wanosimama unless (labda) anasema anapita jumla lakini tuwe na uhakika anapita kweli jumla, lakini kama watasimama Morogoro tuwe na uhakika wa Afya zao” alisisitiza Sanare.
Katika kutekeleza azma hiyo Mkuu huyo wa Mkoa alimtaka Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Kusilye Ukio kuandaa utaratibu wa kitaalamu wa kuweka wataalamu wa kupima dalili za ugonjwa huo kwa wasafiri wote wanaoingia ndani ya Manispaa ya Morogoro ikiwa ni pamoja na barabara ya kutoka Dar es Salaam, Barabara ya kutoka Dodoma na Barabara ya kutoka Iringa.
Sambamba na lengo la kujiwekea mikakati ya kupambana na ugonjwa wa CORONA, Mkuu wa Mkoa pia alitoa wito kwa wadau hao kuwa na michango mbalimbali ikiwa ni maandalizi ya kukabiliana na homa hiyo endapo itaingia katika Mkoa wito ambao ulipokelewa na wengi wao waliahidi kutoa fedha, vifaa tiba na vifaa kinga.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alisema kwa kuwa jambo hilo linatakiwa kufanyika kwa haraka wadau wawe na siku maalum kwa wao kutoa michango yao kama walivyoahidi na kukubaliana Aprili 24 mwaka huu kuwa ndiyo siku ya wote kutoa michango waliyoahidi. Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo aliweka bayana Akaunti ya Benki itakayotumika katika kukusanya michango hiyo kuwa ni ACC. NO. 24910000541 benki ya NMB kwa jina la RAS MOROGORO MAAFA ACCONT.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare(kushoto) akipokea msaada wa mashine ya kusaidia mgonjwa kupumua (haipo pichani) iliyotolewa na mmoja wa wadau wa kikao hicho. kutoka kulia ni ndg Beratus Sambili aliyetoa msaada wa mashine hiyo, Mhe. Pascal Kihanga Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na Mhandisi Emmanuel Kalobelo ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kusilye Ukio (kushoto) akipokea mashine ya kusaidia mgonjwa kupumu kutoka kwa Mdau wa kikao hicho ikiwa ni jitihada za kukabiliana na ugonjwa wa CORONA.
Mwisho, Loata Sanare alitoa onyo kwa wadau walioshiriki kikao hicho, akiwataka wote kutekeleza magizo ya Serikali na ushauri unaotolewa na Wataalamu wa Afya katika jitihada za kutokomeza gonjwa hilo. Amesema mjumbe wa kikao hicho hata kama atakuwa ametoa mchango mkubwa wake, lakini kama eneo lake la kufanyia kazi litakuwa halina tahadhali ya kujikinga na ugonjwa wa CORONA serikali haitasita kuchukua hatua ya kufunga huduma inayotolewa na mdau huyo.
Nao wajumbe wa kikao hicho, kwa nyakati mbalimbali wakichangia mjadala huo walishauri Serikali ngazi ya Mkoa kuongeza jitihada za kuzuia mikusanyiko ya watu isiyokuwa ya lazima katika maeneo mengi ndani ya Mkoa huo hususan katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kuwa wengi wao wanaonekana kutotilia maanani suala nzima la kuwa na tahadhari ya homa hiyo.
Naye Mmiliki wa vyombo vya habari vya TV Imani, Redio Imani na gazeti la Imani (Islamic foundation) Aref Nahd alishauri vyombo vya habari vitumike katika kuendelea kusisitiza masuala mbalimbali yanayotolewa na Serikali, namna ya kujikinga na CORONA akiamini kuwa watu wengi watapata Elimu ya kujikinga na ugonjwa huo kupitia Media.
Kwa upande wa Viongozi wa dini walioalikwa katika Kikao hicho, kwa niaba ya viongozi wenzake Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro Mhashamu Telesphori Mkude alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuandaa kikao hicho kilichowapa ufahamu wa hali ya ugonjwa wa CORONA Mkoani humo na kupata Elimu mbalimbali ya namna ya kujikinga.
Hata hivyo Askofu Mkude alisema katika kuitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wa kuwa na siku tatu za kuliombea taifa kuhusu ugonjwa wa CORONA, alisema, Kanisa Katoliki Kupitia Makao yake Makuu ya Kanisa hilo hapa nchini (TEC) yaliyopo jijini Dar es Salaam wamepanga kufanya Novena ya siku tisa kuanzia Aprili 25 mwaka huu kwa lengo la kuiombea nchi kuepukana na janga la ugonjwa huo.
Wataalamu wakionesha wadau wa kikao baadhi ya vifaa kinga vya gonjwa la CORONA vinavyohitajika
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.