Na. Andrew Chimesela - Morogoro
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi Regina Chonjo amemtaka Chifu wa kabila la Waluguru Mkoani Morogoro Chifu Kingalu Mwanabanzi wa 15 kusimamia na kutunza mila na desturi za kabila hilo ili kurithisha kizazi cha sasa na kijacho utamaduni wa kabila hilo.
Mkuu huyo wa Wilaya ametoa ushauri huo leo Novemba 6 mwaka huu wakati akikabidhi vifaa vya mila na desturi vya kabila la waluguru ambavyo vilipotea miaka 30 iliyopita katika mazingira ya kutatanisha ambavyo sasa vimepatikana baada ya Mkuu huyo wa Wilaya kuwaita Wazee wa Mila na Desturi Mkoa wa Morogoro kufika Ofisini kwake ili kuvitambua vifaa hivyo.
Bi. Regina Chonjo amesema ni vema vifaa hivyo vilivyokuwa vimepotea vitunzwe na kufanya kazi yake na si kuvihifadhi pekee ili kuendelea kutunza utamaduni wa kabila la Waluguru, historia ya Waluguru na kwa kufanya hivyo nchi itaendelea kutunza utamaduni wake kupitia makabila machache yanayoendelea kutunza mila na utamaduni wao.
“lakini naomba msiende kuviweka ndani ili historia ya waluguru isife kwa sababu tunasema taifa lisilokuwa na utamaduni wake lisilokuwa na asili ni sawa na taifa ambalo halipo” alisema Bi. Regina.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema kizazi cha sasa na kijacho kikijua mila na desturi za wazee wetu, vitu vilivyoheshimiwa, taratibu zilizokuwa zinafuatwa na mambo yaliyokuwa yanakatazwa kufanywa na makabila mbalimbali hapa nchini itasaidia kutunza maadili ya wanamorogoro na watanzania wote kwa jumla.
Akiongea katika tukio hilo la kukabidhiwa vifaa hivyo, Chifu Kingalu Mwanabanzi wa 15 kwanza amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuwaita Ofsini kwake kutambua vifaa hivyo vya mila na desturi vya kabila lao na kwamba vifaa hivyo vilipotea mwaka 1988 kwa kuibwa enzi za utawala wa chifu Kingalu Mwanabelege wa 12 aliyetawala kati ya mwaka 1954 hadi 1991.
Hata hivyo Chifu Kingalu Mwanabanzi wa 15 akipokea vifaa hivyo amesema mila ya Kabila la waluguru bado inafanya kazi na iko hai kwa maana ya kuwepo mawasiliano ya moja kwa moja kati yao na kile wanachokiamini hivyo hawako tayari kuvidharau vifaa hivyo vya kimila na kuahidi kuvirudisha katika himaya ya kichifu.
Naye Mlezi na mshauri wa Shirika la wazee wa Mila na Desturi Mkoa wa Morogoro Bw. Mlenge Pakalapakala, amesema ataendelea kushirikiana na wazee hao na kutoa ushauri ufaao kwao ili kurudisha maadili ndani ya jamii ambayo yameonekana kuendelea kuporomoka kila kukicha kwa sababu ya jamii kudharau mila na desturi za wahenga wetu.
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.