DED Kilosa apewa siku 13 kuwapa maji wananchi wa Ruaha
Na Andrew Chimesela – Ruaha, Morogoro
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa ametoa wiki mbili kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuhakikisha anawapatia maji safi na salama wananchi wa Kata ya Ruaha iliyopo katika Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.
Waziri Majaliwa ametoa agizo hilo leo Septemba 17 alipokuwa anaongea na wananchi wa Kata ya Ruaha wakati wa ziara yake ya siku nne Mkoani Morogoro akiwa njiani kuanza ziara ya siku moja Wilayani Kilosa kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya hiyo.
Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya kibaoni akitoa taarifa ya kituo hicho kwa Mhe. Waziri Mkuu
Akianza ziara Wilayani humo, Waziri Mkuu alipokea kero ya maji kutoka kwa wananchi wa kata ya Ruaha kwamba ni ya muda mrefu. Mhe. Waziri Awali Waziri Mkuu alitaka kujua kutoka kwa Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Kilosa Joshi Chumu namna walivyolishughulikia suala hilo na gharama inayotumika katika kuchimba kisima kifupi cha maji.
Mhandisi Chumu alimueleza Waziri Mkuu kuwa uchimbaji wa kisima kifupi cha maji hadi kukamilika kwake kinagharimu kiasi cha shilingi milioni 30 na kwamba kazi hiyo inachukua siku mbili hadi kukamilika kwake.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt.Stephen Kebwe akitoa akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi wa Kibaoni Ifakara
Aidha, Waziri Mkuu alitaka pia kujua kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale kiasi cha fedha zilizopo sasa katika Halmashauri yake ambazo zinazotokana na makusanyo ya ndani ya Halmashauri na kuambiwa fedha zililizopo hadi muda huo zilikuwa shilingi milioni 70.
Waziri Mkuu akianfgalia maelezo na mipango ya Upanuzi wa kiwanda cha Sukari cha Kilombero alipotembelea leo Septemba 17
Baada ya maelezo hayo kutoka kwa viongozi hao Mhe Waziri Mkuu akatoa agizo kutumia fedha hizo zote kwa maana ya shilingi milioni 70 zilizopo sasa, zitumike kuchimba visima vifupi vya maji kwa lengo la kuwapatia maji safi na salama wananchi wa kata ya Ruaha kama ufumbuzi wa kero hiyo ya maji kwa muda mfupi na kazi hiyo ikamilike kabla au ifikapo Septemba 30 mwaka huu.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akiongea na wananchi wa Kata ya Ruaha Wilayani Kilosa
Kabla ya kufika eneo la Ruaha leo hii Waziri Mkuu alikuwa amekwishatembelea kituo cha Afya cha Kibaoni katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara na Kiwanda cha Sukari cha Kilombero. Kesho Septemba 18 Mhe Waziri Mkuu anatarajia kukamilisha ziara yake Mkoani Morogoro kwa kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro DC.
Ni sehemu ya wakazi wa Ruaha wakimsikiliza Waziri Mkuu
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.