Na. Andrew Chimesela, Morogoro
Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Florent Kyombo kusimamia kwa karibu watumishi wa Idara ya ardhi wa Halmashauri hiyo ili kuimarisha kasi ya kutoa huduma kwa wananchi wa Wilaya hiyo.
Waziri Lukuvi ametoa agizo hilo Novemba 9 mwaka huu wakati wa ziara yake ya siku moja katika Halmashauri hiyo na kubaini kile alichokiita utendaji usioridhisha wa watumishi wa idara ya ardhi jambao linalopelekea kuchelewesha utoaji huduma kwa wananchi wa Halmashauri hiyo pamoja na kuikosesha Serikali mapato.
“Mkurugenzi simamia ofisi yako, simamia watumishi hawa wa idara ya ardhi wanakuchafua sana na kukufanya uonekane hufai kwa wananchi, usipofanya hivyo utasababisha matatizo makubwa na kupelekea Serikali ionekane ya ovyo”, alisema Waziri Lukuvi.
Utendaji mbovu kwa watumishi wa idara ya ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ulibainika pale Waziri Lukuvi alipotembelea ofisi ya idara ya Ardhi na kujionea mlundikano wa mafaili zaidi ya 300 ya wananchi yanayosubiri kupatiwa hati za umiliki wa ardhi huku mengine yakionesha kuwepo ofisini hapo kwa zaidi ya miaka mitatu licha ya kutimiza vigezo vyote vya kupata hati.
Kufuatia hali hiyo Waziri Lukuvi amewataka watumishi wa idara ya Ardhi katika Halmashauri hiyo kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka huu wawe wametoa hati miliki za ardhi kwa wananchi wote wanaosubiri hati hizo ili wawe wamiliki halali wa ardhi zao na kuipatia Serikali mapato kupitia kodi ya ardhi.
Aidha, Waziri Lukuvi amewaonya watumishi wa idara hiyo kutofanya kazi kwa mazoea badala yake wafanye kazi kwa kufuata Sheria, kanuni na taratibu zilizopo pamoja kutenda haki bila kumuonea mtu, na atakayebainika kutofuata maagizo hayo atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Awali akimkaribisha Waziri Lukuvi kuongea na watumishi wa Idara ya ardhi, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mwalimu Mohammed Utali, amekiri kuwepo kwa matatizo ya ardhi katika Halmashauri yake yanayosababishwa na baadhi ya watumishi wa idara ya Ardhi wasiofuata kanuni na sheria katika utendaji wao wa kazi.
Amesema, wapo watumishi wanaothubutu kuwakatisha tamaa wananchi kwa kuwaambia kuwa Mkuu wa Wilaya hana ardhi isipokuwa wao ndio wenye mamlaka ya kutoa ardhi jambo linalopelekea kuchelewesha utoaji huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya MvomeroFlorent Kyombo amesema, ujio wa Waziri Lukuvi umebainisha changamoto lukuki zilizopo katika idara ya ardhi katika halmashauri yake na kuahidi kusimamia ipasavyo utendaji wa watumishi wa idara hiyo ili wawajibike ipasavyo.
Katika hatua nyingine Waziri Lukuvi amerejesha shamba namba 25 la Wami Luhindo kwa mmiliki wake Bi. Secilia Lusimbi baada ya shamba hilo kufutwa pasipo kufuata utaratibu na kumtaka mmiliki huyo kuendelea na shughuli zake katika shamba lake na kulipa Serikalini kodi zote zinazostahili kutokana na kumiliki shamba hilo.
Akiongea mara baada ya kurejeshewa shamba lake Bi. Secilia Lusimbi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kwa kumrejeshea shamba lake kwa kuwa amezungushwa kwa muda mrefu na baadhi ya watu waliokuwa na nia ya kuzuia haki yake.
Waziri Lukuvi amekamilisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Morogoro baada ya kutembelea Halmashauri za Wilaya ya Kilosa na Mvomero kwa lengo la kushughulikia changamoto zilizojitokeza katika sekta ya ardhi katika Wilaya hizo.
MWISHO
Haki Miliki © 2018 Mkoa wa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa