Na. Andrew Chimesela - Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen kebwe ameutaka Uongozi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa NIDA Mkoani humo kuongeza Idadi na kusogeza karibu na wananchi vituo vya kusajili wananchi ili kongeza kasi ya utoaji namba na vitambulisho vya Taifa.
Dkt. Kebwe ametoa agizo hilo Kauli hiyo Agost 21, mwaka huu alipofanya ziara ya kushtukiza katika Ofisi za NIDA Mkoani humo zilizopo eneo la Tungi nje kidogo na Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kujionea kasi ya utendaji kazi kulingana na muda uliobaki wa kukamilisha zoezi la kusajili kadi za simu kwa kutumia kitambulisho cha Taifa.
Akitoa maagizo kwa Viongozi wa NIDA Ofisini hapo, Mkuu wa Mkoa amewataka kusogeza karibu huduma hiyo kwa wananchi hasa kwa kuzingatia bado idadi kubwa ya wakazi wa Morogoro hawajasajiliwa kutokana na kituo cha NIDA kuwa kimoja.
“Natoa maagizo kwenu viongozi muhakikishe mnafungua Ofisi nyingine eneo la mjini ili kusogeza karibu huduma kwa wananchi, yapo majengo ambayo mnaweza kuyatumia kwa sasa kama pale stendi ya Msamvu na jengo la zilizokuwa Ofisi za Halmashauri ya Morogoro vijijini”,
Alisema.
Dkt. Kebwe. ameitaka Mamlaka hiyo kumpa taarifa endapo kuna sehemu inahitaji msaada kutoka Uongozi wa Mkoa ili kuhakikisha shughuli za usajili zinakamilika kwa wakati.
Sambamba na hayo Dkt. Kebwe amewataka wataalamu wa NIDA kuongeza kasi ya utendaji kazi hususan katika zoezi la utoaji namba za vitambulisho ili kuwarahisishia wananchi kukamilisha mahitaji yao mbalimbali ikiwemo usajili wa namba za simu.
Amesema zipo Halmashauri Mkoani humo ambazo zoezi hilo linakwenda vyema lakini akasisitiza kuongeza juhudi kwa baadhi ya Halmashauri ambazo utekelezaji wake wa zoezi hilo si wa kuridhisha ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijni.
Kuhusu sualala utoaji Elimu kwa wananchi juu ya zoezi hilo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ameitaka NIDA Mkoani humo kushirikiana na vyombo vya habari vilivyopo ndani ya Manispaa ya Morogoro ili kufikisha elimu kwa wananchi walio wengi.
Pamoja na hayo Mkuu wa Mkoa ameyataka makampuni ya mawasiliano ambayo hayajaweka vituo vyake vya kusajili laini za simu nje ya jengo la Ofsi za NIDA Mkoani humo kuhakikisha wanaweka vituo hivyo lengo likiwa ni kumwezesha mwananchi kupata huduma ya kusajili namba zao za simu punde tu anapopata kitambulisho chake cha Taifa.
Kwa upande wake Afisa Msajili Mfawidhi wa NIDA Mkoa wa Morogoro James Malimo amesema wamepokea maagizo ya Mkuu wa Mkoa na watayatekeleza huku akiahidi kuwa kufikia Jumatatu ya tarehe 26 mwezi huu watafungua kituo kingine katika maeneo jirani na wananchi ikiwemo katika jengo la zilizokuwa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kama walivyoelekezwa na Kiongozi wao.
Amesema katika zoezi hilo la Usajili tayari asilimia 90 ya wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wameshasajiriwa huku waliopata namba za vitambulisho ni asilimia 75.
Mwezi Aprili mwaka huu akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Mbeya, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliitaka Mamlaka ya Mawasiliano Nchini TCRA kutowabugudhi wananchi ambao hawatoweza kusajili laini zao za simu hadi kufikia mwezi Mei na kuagiza zoezi hilo lisogezwe mbele hadi mwezi Disemba mwaka huu kutokana na Watanzania walio wengi kutokuwa na vitambulisho vya Taifa.
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.