Kebwe awatuliza Wakazi Mindu
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amewatoa hofu wananchi wa Kata ya mindu wanaoishi karibu na Bwawa la Mindu kwa kuwataka wawe watulivu wakisubiri maelekezo kutoka Serikalini kuhusu changamoto inayojitokeza katika eneo wanaloishi.
Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo jana Februari 20, 2019 wakati anazaungumza na wananchi wa Mitaa mitatu ya Kata ya Mindu wanaokaa karibu na Bwawa hilo kwa lengo la kuwafikishia ujumbe Mawaziri Nane waliotembelea Bwawa hilo hivi karibuni na kuangalia changamoto ya sheria ya mita 60 na mita 500 kwa wakazi na shughuli za kibinadamu zinaendeshwa jirani na bwawa hilo.
Katika ziara hiyo ambapo wakazi wengi walionekana kupatwa na mshtuko wakidhani Mkuu huyo wa Mkoa amepeleka ujumbe tofauti na ule uliotolewa na timu ya Mawaziri Nane waliofika katika bwawa hilo hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa aliwatoa hofu kuwa yeye hana jambo jingine jipya.
“Kwa hiyo tumeona tuje tuwatoe hofu wananchi kuhusu hili wala hakuna jambo jingine lolote lile” alisema Dkt. Kebwe
Hata hivyo Dkt. Kebwe aliwatahadharisha wananchi hao kutojimilikisha maeneo katika eneo hilo wala kudanganywa na mtu au watu kwa kuuziwa viwanja katika eneo hilo ambalo maamuzi yake yanasubiriwa kutolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli.
“Hili liko mikononi mwa Mwenye nchi, asije akatokea mtu akawaambia jamani hapa kuna kipande cha shilingi laki moja au shilingi laki mbili, tujihadhari kwa hilo” aliongeza Dkt. Kebwe
Awali timu ya Mawaziri Nane ikiongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ilitembelea Bwawa hilo na ikatoa maelekezo kwa Mkoa kusimamisha programu yoyote inayoendelea katika eneo hilo ikiwa ni pamoja na ile ya kutaka kuwahamisha wakazi wa eneo hilo hadi hapo watakapopewa maelekezo kutoka Serikalini huku ikiwataka pia kuzuia watu wasiendelee kuongezeka katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Ofisa wa Bodi wa Bonde la Wami Saimoni Ngonyani alibainisha kuwa Bwawa la Mindu ambalo linachangia kwa asilimia 80 ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro limekubwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupungua kwa kina kunakosababishwa na shughuli za kibinadamu zinazofanyika katika maeneo ya karibu na bwawa hilo.
Afisa Habari
RS Morogoro
20 Februari, 2019
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.