RC Sanare aitaka Kilosa “kufunga mkanda” ukusanyaji mapato
Na, Andrew Chimesela, Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kuongeza nguvu katika kukusanya mapato ya ndani kutoka katika vyanzo vyake badala ya kutegemea fedha za kuendesha Halmashauri hiyo kutoka Serikali Kuu.
Sanare ametoa rai hiyo Mei 6 mwaka huu wakati wa baraza maalum la madiwani kwa ajili ya kujadili taarifa na majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali za mwaka wa fedha 2018/19.
RC Sanare (mwenye tai nyekundu) akiongoza Kikao cha Baraza Maalum la Madiwani Halmashauri ya Kilosa Mei 6, 2020
Amesema, Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha imekusanya asilimia 50 tu ya makadirio yake hivyo Halmashauri imeshindwa kutekeleza malengo yake ya kukusanya mapato.
“Mmeshindwa kukusanya mlichosema tutakusanya, hii ndio tafsiri yake lakini ukiingia kwa undani ukifika madukani watu wanafanya biashara hawana leseni utapataje sasa fedha hizo mnazosema mtakusanya” alihoji Sanare.
Malengo ya kukusanya mapato ya ndani ilikuwa zaidi ya shilingi 5.6 Bil. Kutoka vyanzo vya ndani lakini Halmashauri hiyo imekusanya shilingi 3.1Bil. pekee na kutofikia azma ya Serikali ya kila Halmashauri kukusanya si chini ya asilimia 80, amesema kwa kipimo hicho Halmashauri imeshindwa kutekeleza maazimio waliyojiwekea.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Eng. Emmanuel Kalobelo akifafanua lengo la kikao cha Baraza maalum
Kwa sababu hiyo ameitaka halmashauri kujiwekea mikakati thabiti ya kukusanya fedha kutoka vyanzo vyake vya ndani ikiwa ni pamoja na kuwataka wafanyabiashara wote kulipa tozo stahiki na kuwasimamia watendaji wa vijiji na Kata kuongeza jitihada za kukusanya mapato ya Halmashauri.
Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilosa kupitia upya watumishi wanaokaimu Ukuu wa Idara kwa muda mrefu, amemtaka afanye mchakato wa ama kuwathibitisha kuwa Wakuu wa Idara kamili au kuwaondoa katika nafasi hizo hususan wale wasiofaa badala ya kuwakaimisha kwa muda mrefu.
Akihitimisha hotuba Loata Sanare amewakumbusha madiwani wa Halmashauri hiyo kutoa Elimu kwa wananchi wao kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa CORONA na kufuata maelekezo yanayotolewa na Wataalamu wa Afya. Kuhusu sakata la sukari, amewataka Wakuu wa Wilaya Mkoani humo, kwanza kufuatilia bidhaa hiyo kupatikana lakini pia kuuzwa kwa bei elekezi na wafanyabiashara watakaouza tofauti na bei hiyo wachukuliwe hatua stahiki.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo alieleza lengo la kikao hicho cha Baraza Maalum la Madiwani kuwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali ambayo inawataka Wakuu wa Mikoa wote hapa nchini kuwa na vikao na Madiwani mara tu baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kukamilisha na kuwasilisha ripoti ya ukaguzi huo.
Aidha, alisema kikao hicho kinalenga kuona na kupitia hoja na maelekezo ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali kwa kila hoja na majibu na mipango iliyojiwekwa na Baraza la wahe Madiwani kuhusu taarifa hiyo na mikakati waliyoitoa.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kutoa hotuba yake, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi aliwataka Wahe. Madiwani wa kutotetea ubadhilifu wowote wa mapato ya Halmashauri hiyo kwa kuwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na sera za Serikali iliyoko madarakani ambayo inasisitiza sana suala la ukusanyaji wa mapato.
DC Kilosa Adam Mgoi akitoa nasaha kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale ameahidi kuzingatia sheria na kanuni mbalimbali za kukusanya na kutumia fedha zitakazokusanywa ndani ya Halmashauri yao.
Ameongeza kuwa Halmashauri yake kwa kushirikiana na Wahe. Madiwani watajitahadi kuzingatia ushauri na maelekezo yaliyotolewa na Mkaguzi Mkazi wa Hesabu za Serikali ili kupunguza au kumaliza kabisa hoja zinzojitokeza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa
Kwa mujibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkazi, amesema jumla ya Halmashauri 299 zilikaguliwa hapa nchini, zilizofanya vizuri ni Halmashauri 176 ikiwemo Halmashauri ya Kilosa.
Kwa upande wa Kilosa amesema Kabla ya mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Kilosa ilikuwa na jumla ya maoni 56 ya kutekeleza. Manoni 51 kati ya hayo yalitekelezwa na kubaki maoni 5. Na kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kulikuwa na jumla ya maoni 37 ya kutekelezwa, kati ya hayo maoni 30 yalitekelezwa kikamilifu na maoni 7 tu ndiyo hayakutekelezwa hii ni sawa na asilimia 81.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.