Onyo la kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa.
Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amewataka Wananchi wa Mkoa huo na watu wote wanaoingia ndani ya Mkoa wa Morogoro kutovamia kwa makusudi maeneo oevu, Hifadhi za misitu kwa kisingizio cha kuruhusiwa na Serikali na kwamnba atakayefanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
Dkt. Kebwe ametoa onyo hilo wakati wa kikao chake na waandishi wa Habari jana Januari 21 Ofsini kwake akitoa tahadhari kulingana na uwepo wa makundi makubwa ya wakulima na wafugaji kuingia Mkoani humo hususan Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi wakidai kuwa Serikali imeruhusu kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo jambo ambalo amesema ni upotoshaji wa maelekezo ya Serikali.
Akifafanua maelekezo ya Serikali, Dkt. Kebwe amesema, Serikali ilitoa maelekezo ambayo hayakuwa na utata kuwa, Serikali kupitia Wiazara husika ndani ya mwezi mmoja zitakaa pamoja na kuangalia maeneo ambayo yamepoteza hadhi ya kuwa hifadhi yatatolewa kwa wananchi kwa utaratibu utakaotolewa.
“Maelekezo ya Serikali yalivyotolewa katika kipindi cha mwezi mmoja Wizara husika zitakaa chini zitatoa maelekezo vizuri na kuainisha maeneo yale ambayo yameshapoteza hadhi ya kuwa hifadhi yaweze kuondolewa na kutolewa kwa wananchi, lakini maeneo yale ambayo bado yana umuhimu wa uhifadhi yaweze kubaki kuendeleza hifadhi zetu” alisema Dkt. Kebwe
Dkt. Kebwe amesema kuna wananchi wakorofi ambao wametafsiri tofauti maelekezo hayo kwa makusudi na kuanza kuvamia maeneo hayo kwa kisingizio cha kuruhusiwa na kuwataka watu hao kuacha mara moja uvamizi huo au kuwa na subira hadi Serikali itakapotoa mwongozo wa namna ya kuyapata maeneo yale ambayo yataonekana yamekosa hadhi ya kuwa hifadhi, vinginevyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Hata Hivyo Dkt. Kebwe amewataka Wakuu wa Wilaya zote Mkoani humo kutoa Elimu katika suala hilo kabla hawajawachukulia hatua za kisheria wale watakaokaidi maelekezo ya kuvamia maeneo ya Hifadhi na maeneo oevu likiwemo Bonde la Mto Kilombero ambalo sasa lina ukubwa wa Km za Mraba 2,190 tu ambapo kabla ya kumegwa na kurasimishwa kuwa makazi ya watu lilikuwa na km za mraba 6500.
Haki Miliki © 2018 Mkoa wa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa