Na Andrew Chimesela – Morogoro,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh. Selemani Jafo ametoa mwezi mmoja kwa uongozi wa Wilaya ya Kilosa kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mikumi baada ya kuonekana kasi ya ujenzi huo kusuasua.
Waziri Jafo ametoa agizo hilo Januari 2 mwaka huu alipofanya ziara ya siku moja wilayani Kilosa Moani Morogoro ambapo ametembelea ujenzi wa kituo cha Afya cha Mikumi, mto Ruhembe unaolalamikiwa na wananchi kupoteza maisha ya watu hususan kipindi cha masika na kuhitimisha ziara hiyo kwa kutembele Kituo cha Afya cha Kidodi.
Amesema fedha za Ujenzi wa Kituo hicho cha Afya Mikumi zilipelekwa mwishoni mwa mwezi Juni 2018 na ujenzi wake ulitakiwa kukamilika mwezi Novemba, 2018 hata hivyo ujenzi huo hadi sasa bado unasuasua hivyo kutoa mwezi mmoja kwa uongozi hadi Januari 30 mwaka huu ujenzi huo uwe umekamilika.
“lakini vile vile barua ni jambo la kwanza ninyi pale mmechelewa sana itakapofika tarehe thelathini mwezi wa kwanza nikute majengo yote yale yawe yamekamilika, kuta zimepandishwa kila kitu nitakuja mwenyewe kukagua majengo yale” amesema Waziri Jafo.
Katika hatua nyingine Waziri jafo amepongeza ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kidodi kwa kuwa ujenzi wake umekamilika kwa wakati ingawa bado kuna mapungufu madogo ya kumalizia na akaagiza kukamilisha mapungufu hayo ifikapo Januari 15 mwaka huu.
Kwa upande wa ujenzi wa daraja la mto Ruhembe ambao upo Tarafa ya Mikumi unaolalamikiwa na wananchi wa eneo hilo kusababisha vifo vya watu unapojaa maji hasa kipindi cha masika Waziri huyo ameahidi kulibeba suala hilo kwa uzito na kwamba ataangalia namna ya kulifanyia kazi ili kutatua changamoto hiyo.
Katika ziara hiyo Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mhe. Joseph Haule amemshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya na akatumia fursa hiyo kuiomba serikali iendelee kusaidia Jimbo la Mikumi na Wilaya ya Kilosa kwa Jumla hususan sekta ya Afya.
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.