KAMATI YA SIASA MOROGORO WAWAFARIJI WAHANGA WA MAFURIKO
Na Andrew Chimesela
Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Morogoro, wamewatembelea na kuwafariji kwa kutoa misaada kwa wahanga wa mafuriko yaliyotokea katika Kijiji cha Dakawa Wilayani Mvomero yaliyotokanana na Mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini.
Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake Innocent Kalogeresi wamewatembelea wahanga hao Februari 7 mwaka huu baada ya kukatisha kwa muda ziara yao ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoteklelezwa ndani ya Mkoa huo.
Baada ya kufika eneo la tukio, Mwenyekiti Innocent Kalogeresi amewapa pole wananchi waliopatwa na kadhia hiyo huku akiwataka wananchi ambao bado wako maeneo ya mabondeni ambayo ni hatarishi kuondoka kwenye maeneo hayo ili kunusuru maisha yao.
“ombi langu pengine kwa namna moja ama nyingine wapo ndugu rafiki ambao bado wanang’ang’ania kuwa kule waambieni waje mahali ambapo pako salama, mto wami una mamba wengi pengine kuendelea kubaki kule tunaweza kupata ajali nyingine ambayo haina sababu” ameonya Kalogeresi
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amewataka wananchi ambao nyumba zao zimezingirwa na maji kutorudi haraka kwenye makazi yao kwani amesema nyumba hizo zinaweza kuanguka kwa sababu ya kuta zake kulowa maji na kusababisha madhara makubwa kuliko ya sasa.
.Kwa sababu hiyo, Mhandisi Kalobelo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amesema ataunda timu ya wataalamu kwenda eneo la tukio na kufanya tathmini ya kina ili kujua usalama wa nyumba zilizolowa maji na kutoa taarifa kwa wenye nyumba hizo kama wanaweza kurudi katika makazi yao ama la, kwa lengo tu la kulinda na kuokoa maisha yao.
“tahadhari yangu, tusiingie haraka haraka kwenye nyumba hizi ambazo zimeingiwa na maji ili tujihakikishie usalama wake” alishauri Mhandisi Kalobelo
Pamoja na ushauri wa pande hizo mbili, Kamati hiyo ya siasa baada ya kuguswa na tukio hilo imekabidhi msaada wa chakula na misaada mingine kwa wahanga waliokuwa kwenye Kambi iliyokuwa imeandaliwa na Serikali ngazi ya Wilaya kushirikiana na Mkoa.
Misaada iliyotolewa ni pamoja na mchele, unga wa ngano, unga wa sembe, mafuta ya kula pamoja na maharagwe huku Katibu Tawala wa Mkoa akitoa wito kwa taasisi zote za Serikali na binafsi ndani ya Mkoa huo kushirikiana pamoja kuwasaidia wahanga waliopatwa na mafuriko hayo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Florent Kyombo, amesema kaya 355 zenye jumla ya wananchi zaidi ya 800 zimeathirika na mafuriko hayo yaliyotokana na mvua zilizonyesha mikoa ya kaskazini hususan Mkoa wa Manyara usiku wa kuamkia Februari 6 mwaka huu na maji yake kuathiri eneo hilo la Kijiji cha Dakawa.
Kamati ya siasa iliendelea na ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Kilosa, ambapo pamoja na miradi mingine ilitembelea mradi wa ukarabati wa shule ya Sekondari ya Kilosa na baadae ikawasili Wilayani Gairo.
hili ni moja ya majengo ya shule ya Sekondari ya Kilosa yaliyokarabatiwa.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.