Wafanyakazi Morogoro wampongeza Rais kurejesha kikokotoo cha zamani, wamuomba kumulika Sekta Binafsi.
Na Andrew Chimesela – Morogoro
Wafanyakazi mbali mbali wa Umma na wasio wa Umma Mkoa wa Morogoro, leo Januari 11, 2019 wameungana na kufanya maandamano ya Amani yaliyolenga Kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kwa kurejesha kikokotoo cha zamani cha mafao ya wastaafu.
Maandamano hayo ambayo yameanzia Ofisi za Vyama vya Wafanyakazi Barabara ya Stesheni hadi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, yamepokelewa na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Kebwe Stephen Kebwe ambaye pia alikuwa Mgeni rasmi.
Katika Risala yao iliyosomwa na Katibu washirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA) Mkoani Morogoro Abubakari Rashidi, Wafanyakazi hao wamesema kuwa hatua ya Mhe. Rais ya kurejesha kikokotoo cha zamani kutumika hadi mwaka 2023 ni cha huruma, busara na kinaoonesha upendo wake kwa wafanyakazi, huku wakimuomba Rais kuangalia kikokotoo kinachotumika kwenye mifuko ya Sekta Binafsi.
“Tunaendelea kumuomba Mhe. Rais atupie jicho lake lenye huruma kwenye mifuko ya mafao yanayotolewa na mifuko ya Sekta binafsi nchini… inayolipa mafao kidogo 25% ambapo inalenga wafanyakazi waliopo Sekta Binafsi na kulipwa mafao kidogo licha ya usawa katika uchangiaji” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Akiongea mara baada ya kupokea maandamano hayo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amewataka wafanyakazi kuiishi kaulimbiu ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli ya “hapa kazi tu” kwa kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na nidhamu ya hali ya Juu.
Aidha, amewataka wafanyakazi kuondoa dhana potofu ya kujenga maisha yao kwa kutegemea mafaao ya baada ya kustaafu bali waaze kujenga maisha yao kuanzia sasa kwa kutumia njia nyingine kama kupata mikopo kwenye taasisi za kibennki na fedha zinazotokana na mafao zitakuja kumsaidia mfanyakazi wakati hana nguvu ya kufanya kazi na hana kipato kingine.
Sambamba na hilo Mkuu wa Mkoa Dkt Kebwe amewaagiza viongozi wa TUCTA kumpelekea orodha ya taasisi/makapuni ambayo hayaruhusu wafanyakazi wake kujiunga na mifuko ya kijamii ili aweze kuyachukulia hatua za kisheria kwani kutofanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi na kuwanyonya wafanyakazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Morogoro Bw. Mohamed Simbee amesema pamoja na kumpongeza Rais kwa kurejesha kikokotoo cha zamani wanamuomba Mhe. Rais aendelee kuangali namna ambayo kikokotoo hicho kutoishia mwaka 2023 bali kiwe endelevu hata baada ya mwaka 2023.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.