KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU ASIFU TARURA – IFAKARA
Na. Andrew Chimesela - Ifakara
Ikiwa ni siku ya tano tangu Mwenge wa Uhuru kuanza kukimbizwa Mkoani Morogoro leo umekimbizwa katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara na kutembelea miradi saba yenye jumla ya thamani ya shilingi 1.9 Bil. ukiwemo Mradi wa Barabara ya Upogolo yenye urefu wa 1.3 Km.
Baada ya kutembelea Barabara hiyo Kiongozi wa Mbioza Mwenge Kitaifa Ndugu Charles Kabeho amesifu utendaji kazi wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini - TARURA kutoka katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara kutokana na kile alichoita kazi hiyo kinafanana na thamani ya fedha zilizotumika
Charles Kabeho amewamwagia sifa watendaji hao wa TARURA Halmashauri ya Mji Ifakara Julai 25 mwaka huu wakati wa Mbio za Mwenge wa uhuru uliokimbizewa ukitokea katika Halmashauri ya Morogoro DC na kuanza kukimbizwa Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro.
Awali Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge alipofika katika Barabara hiyo alianza kumuuliza maswali mbalimbali Meneja wa TARURA wa Halmashauri ya Ifakara na kupewa majibu ambayo yalimfanya kupima upana wa barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha Changarawe hivyo kutoa tape measure kutoka mfukoni mwaka na kuanza kupima.
Aidha, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru hakuishia hapo alimtaka Meneja huyo, Waandishi wa Habari pamoja na viongozi wengine wa ngazi ya Wilaya akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kilombero James Ihunyo kupanda kwenye magari ili kupima urefu wa barabara hiyo kwa lengo la kujiridhisha kama barabara hiyo ina urefu uliotajwa kwenye taarifa.
Baada ya kukamilika kwa mtihani huo majibu yalitolewa kuwa yanafanana na maelezo yaliyotolewa katika taarifa iliyosomwa kwake awali, jambo lililomsukuma kuwapongeza Viongozi wa TARURA wa Halmashauri hiyo ya Ifakara kwa kusema ukweli na kufanya kazi kulingana na mikataba inavyoelekeza.
“kwanza ninachoweza kuwashauri watendaji wote wanaotekeleza miradi ya maendeleo, wawe wanazingatia viwango vinavyotajwa kwenye mikataba. Lakini pia wasisite kuchukua hatua pale ambapo Mkandarasi anafanya kazi tofauti na mikataba hiyo.alisema Charles Kabeho.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero James Ihunyo alimsifu Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2018 kuwa yupo imara na kumuomba aendelee kusimamie suala zima la mlinganyo kati ya fedha na kazi (Value for money) ili fedha zinazotolewa na Serikali zilete matunda kwa Jamii.
Awali akisoma taarifa ya Mradi huo wa barabara ya Upogolo itakayogharimu zaidi ya shilingi 400 Mil. hadi kukamilika kwake, Meneja wa TARURA Halmashauri ya Mji wa Ifakara Imannuel Mfinanga, alisema eneo la Upogolo lina changamoto ya kujaa maji kipindi cha masika hivyo mradi huo wa barabara unalenga kuondoa changamoto hiyo na kuwawezesha wananchi kupata huduma za mahakama na Kituo cha Polisi kwa kipindi chote cha mwaka.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.