Madiwani watakiwa kuhamasisha ukusanyaji mapato
Na Andrew Chimesela, Morogoro
Baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga limeaswa kuwa na utamaduduni wa kuwahamasisha wananchi wa maeneo yao katika suala nzima la kulipa kodi na michango mingine halali ili kuongeza mapato ya halmashauri hiyo na kusaidia kuleta maendeleo yao.
Rai hiyo imetolewa Mei 19 mwaka huu Wilayani Ulanga na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare wakati wa Baraza Maalum la madiwani la Halmashauri hiyo wakati wa kujadili taarifa na majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Amesema Waheshimiwa madiwani wanalazimika kuwa mfano na kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha wananchi kwenye maeneo yao kuelewa faida ya ukusanyaji wa kodi ili waweze kutoa kodi kwa maendeleo yao badala ya madiwani hao kuwahamasisha wananchi hao kutolipa kodi au tozo mbalimbali.
“Maeneo mengine madiwani wengine ndio shida, wanahamasisha wananchi wavunje utaraibu, wanahamasisha wananchi wasilipe kodi, hii ni shida sana na kwa bahati mbaya sana tunazo taarifa za madiwani wa Kata hizo wanaofanya mambo kama hayo hatutawavumilia” ameonya Loata Sanare.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare akiongoza Kikao cha Baraza Maalum katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Jonas Mallosa kufuata taratibu zote za ukusanyaji na utumiaji wa fedha zinazokusanywa kutoka vyanzo mbalimba vya mapato ya ndani kwamba fedha hizo zikusanywe kwa njia ya kielecktroniki na kisha kupelekwa benki kabla ya kuzitumia.
“Fedha zote Mkurugenzi hakikisha zinaingia benki kwa utaratibu wa elektroniki, hunyimwi kutoa na kutumia unavyotaka wewe, katika maeneo mengi ndani ya halmashauri zetu wanakata hela huko huko juu kwa juu wanawapatia shida vijana wale wanaotukusanyia fedha kwa sababu maelekezo yanatoka kwa Mkurugenzi, maelekezo yanatoka kwa DT maelekezo yanatoka kwa yule jamaa mwingine” amesema Loata Sanare.
DC Ulanga Ngollo Malenya akisikiliza kwa makini hoja zinazotolewa wakati wa Baraza maalum la Halmashauri hiyo, Mei 19 mwaka huu
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewaonya watumishi wa serikali Wilayani ambao hawatoi ushirikiano kwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kutoa ushirikiano unaohitajika kwa kiongozi huyo pindi inapohitajika ili kuleta ufanisi wa kazi yake na kuongeza maendeleo ya Halmashauri hiyo.
Kiongozi huyo ambaye ndiye mwenyekiti wa kikao hicho cha Baraza Maalum la Madiwani kwa ajili ya kutekeleza agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya watumishi hasa wakuu wa Idara, kusababisha kuendelea kwa Hoja zisizo na majibu suala ambalo linaharibu taswira ya utendaji wao na Mkoa kwa jumla.
Baadhi ya wajumbe na waalikwa wa kikao hicho cha Baraza
Katika kikao hicho cha Baraza Maalumu, mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za serikali Mkoa wa Morogoro, ameeleza kuwa pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Ulanga kupata hati inayoridhisha, bado kuna hoja tano zilizokosa majibu.
Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Morogoro CPA Peter Mwabwanga
Miongoni mwa hoja zinazoelezwa kukosa majibu, ni pamoja na Usimamizi wa watumishi, baadhi ya taarifa za manunuzi, taarifa za mikataba mbalimbali toka ofisi ya mwanasheria pamoja na kutozingatiwa kwa baadhi ya maagizo ya serikali.
Makamu Mw wa Baraza la Halmashauri ya Ulanga
Viongozi wa Baraza la Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.