MAJALIWA ARIDHISHWA NA UJENZI - SGR
Na Andrew Chimesela – Morogoro
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa ameonesha kuridhishwa na ujenzi wa mradi wa reli ya mwendo kasi (Standard Gauge Railway – SGR) unaotekelezwa kuanzia kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro hususan ujenzi wa handaki lenye urefu wa kilometa moja linalojengwa Wilayani Kilosa ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 83.
Waziri Mkuu akiwasili kwa Helkopta eneo ambalo handaki limechorongwa kwa ajili ya kupita reli ya SGR, Kilosa Mkoani Morogoro
Waziri Mkuu amesema hayo Mei 14 mwaka huu baada ya kukagua kipande cha mradi huo na kuhitimisha ziara yake kwa kutembelea ujenzi wa handaki hilo lililochorongwa chini ya mlima nje kidogo ya Mji wa Kilosa ili kupitisha Reli ya SGR lengo likiwa ni kukwepa changamoto za mto Mkondoa ambazo mara kadhaa zimekuwa tishio kwa usafiri wa Reli katika eneo hilo.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa pili kulia), akiwa amepokelewa na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare (wa tatu kulia) wakati amewasili Wilayani Kilosa kwa ajili ya kutembelea handaki ambapo reli ya mwendo kasi itapita
Mhe. Kassim Majalwa akiwa ndani ya handaki
Katika hotuba yake fupi aliyoitoa mara baada ya kukagua handaki hilo Mhe. Majaliwa amesema ameridhishwa na ubora, kasi, na hatua iliyofikiwa ya Ujenzi wote wa SGR lakini pia kuridhishwa na kazi kubwa iliyofanywa ndani ya handaki hilo na kuwapongeza Kampuni ya Yarp Merkez iliyochaguliwa kutekeleza mradi huo, Wizara na watendaji wake wote.
Hili ndilo handaki lenye urefu wa zaidi ya 1Km linavyoonekana kwa ndani, ambalo Reli ya mwendo kasi itapita kutoka upande mmoja wa mlima kwenda upande wa pili ili kuivusha reli hiyo kwenye mto Mkondoa.
Handaki livyoonekana kwa nje
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasihi watanzania waliopata kazi katika kampuni ya Yarp Merkez inayojenga reli hiyo kuongeza nguvu katika kufanya kazi ili kukamilisha ujenzi huo kwa muda uliopangwa.
Akizungumzia faida ya reli hiyo Waziri Mkuu amesema mradi huo ni moja ya miradi ya kimkakati utakaokuza uchumi wa nchi lakini pia utaondoa changamoto ya ajira hususan vijana ambapo awali vijana wengi walikuwa wakikaa vijiweni lakini kupitia mradi huo na mradi wa Bwawa la Mwl. Nyerere juma ya vijana elfu 18 wameajiriwa.
Waziri Mkuu akipewa maelezo na Watendaji wa TRC kuhusu ujenzi wa handaki hilo.
Aidha, Waziri Mkuu amesema reli hiyo itakapokamilika itafanya kazi masaa yote kwa kuwa itaendeshwa kwa umeme utakaounganishwa kutoka katika vyanzo vitatu vya uhakika ukiwemo ule unaotoka Bwawa la mwalimu Nyerere, umeme wa Kidatu unaozarishwa kutokana na bwawa la Mtera na umeme wa Kinyerezi unaotokana na gesi hivyo Reli hiyo haisimama kufanya kazi kwa sababu ya kukosa nishati ya umeme.
Ili kuwahakikishia zaidi watanzania Waziri Mkuu amesema, endapo vyanzo vyote hivyo vya umeme umeme wake ukikatika jambo ambalo ni nadra kutokea, bado reli hiyo itaendelea kufanya kazi kwa kutumia mtambo maalum utakaokuwa umefungwa kwenye reli yenyewe ukiwa na uwezo wa kuendesha reli kwa dakika 45.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (katikati) akiwa na mwenyeji wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare (kulia) wakati wa kutembelea handaki la SGR nje kidogo ya Mji wa Kilosa
Akitoa rai kwa watanzania waliopata ajira kwenye mradi huo Majaliwa amewataka kutumia fursa hiyo kwa kujenga uaminifu na kujituma huku akiwataka kujituma kupata ujuzi katika sekta walizopo ili baadae waweze kujiajiri ama kuajiri vijana wengine pamoja na kuomba tenda katika miradi mbalimbali.
Akizungumzia suala la ugonjwa wa CORONA, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare kutoa maelekezo kwa Wakuu wa Wilaya katika Mkoa huo kuendelea kutoa Elimu kwa wananchi juu ya ugonjwa huo namna unavyoenea na namna ya kujikinga kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa Afya lakini amewataka wafanye hayo wakiendelea na kufanya shughuli zao za kila siku.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa ndani ya Helkopta tayari kwa safari ya kurudi Dodoma
Mradi wa Reli ya mwendo kasi ambao umeelezwa kuwa utawanufaisha watanzania kwa kipindi cha miaka 100 ijayo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni mwakani.
mwisho
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.