Mkimbiza Mwenge Kitaifa akataa kukabidhi Hati Miliki za Kimila 250
Na. Andrew Chimesela - Morogoro
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2018 ndugu Charles Kabeho amekataa kukabidhi hati miliki za kimila 250 kwa wananchi wa Kijiji cha Mikese ambacho kipo ndani ya mradi wa Upimaji na Urasimishaji wa Ardhi unaofanyika chini ya Shirika la PELUM Tanzania kwa madai ya taarifa za kifedha za mradi huo zina zina kasoro.
Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge amekataa kukabidhi hati hizo Julai, 24 mwaka huu wakati wa kukimbiza Mwenge wa Uhuru ambao ulikimbizwa katika Kijiji cha Mikese ambapo ratiba ilionesha Kiongozi huyo kutakiwa kukabidhi hati hizo 250 za wananchi wa Kijiji hicho kati ya Hati miliki 750 ambazo ziko tayari kutoka vijiji vingine vya Kata ya Mikese.
Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge Kitaifa alieleza sababu ya kutokabidhi hati hizo kuwa kulikuwa na mapungufu katika utoaji wa gharama zilizotumika kwenye mradi huo huku akibainisha kuwa taarifa zilizoandaliwa na Mkoa huo zinasema gharama ya mradi wa Upimaji na Urasimishaji Ardhi zilizotumika ni shilingi 100 Mil. wakati taarifa za kutoka Halmashauri ya Morogoro zinaonesha gharama gharama zilizotumika ni shilingi 153, 120,000/=
“Mradi wa Upimaji na Urasimisha wa Ardhi kwa Wananchi, taarifa zake za fedha zimekuwa tofauti, Kitabu cha Mkoa kinasema shilingi milioni 100 lakini taarifa husika inasema shilingi 153,120,000/= ongezeko la shilingi 53,120,000/= ni fedha ambazo ni nyingi” alisema Kiongozi huyo.
Amesema Mradi huo ni wa fedha za wahisani zimetolewa ili kuondoa migogoro ya ardhi iliyokithiri Mkoani Morogoro, hivyo sio vema kuacha suala hilo kirahisi huku lina kasoro zinazoonesha kuwa ni za ubadhirifu huku kukiwa na tofauti ya kiasi kikubwa cha fedha.
Kwa sababu hiyo Ndugu Charles Kabeho ameagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuuchunguza mradi huo ili kupata ukweli wake huku akizitaka hati zote zilizotakiwa kukabidhiwa kwa wananchi zisitolewe kwa wananchi husika zihifadhiwe Ofisi ya Usalama ya Mkoa kwa usalama zaidi hadi uchunguzi wa suala hilo utakapokamilika.
Pamoja na maagizo hayo, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge Kitaifa, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro kusimamia suala hilo kwa karibu na endapo uchunguzi utabaini ubadhilifu wa aina yoyote, basi wahusika wote wa sakata hilo wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Akijibu mkanganyiko huo ulivyotokea baada ya kuulizwa swali na Mkimbiza Mwenge Kitaifa, Mratibu wa mbio za Mwenge Kimkoa Mkoa wa Morogoro Bw. Diazi Ndomba amesema taarifa ambayo ipo katika kitabu cha miradi ya Mwenge ya Mkoa huo ililetwa na Halmashauri husika na wao ndio wanaweza kutoa maelezo ya kina kuhusu utofauti huo.
Naye Mratibu wa shirika la PELUM Tanzania Bw. Anglolile Reyson amesema mchakato wote kuhusu suala la Upimaji na Urasimishaji wa Ardhi kwa wananchi wa vijiji vinavyohusika na mradi huo umefuata taratibu zote zinazotakiwa.
Mradi wa Upimaji na Urasimishaji Ardhi kwa wananchi umefanyika katika Kata ya Mikese, na kuhusisha Vijiji vya Mikese, Newland, Lubungo na Mfumbwe. Jumla ya Hati Miliki za kimila 750 zimeandaliwa kutolewa kwa wananchi wa Vijiji vya Mikese hati 250, Newland hati 160, Lubungo hati 175 na Mfumbwe hati 165.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.