Morogoro yaongoza kufanya vema miradi ya Kimkakati, viongozi wapongezwa.
Na Andrew Chimesela - Morogoro
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ameupongeza Uongozi wa Mkoa wa Morogoro kwa kutekeleza vizuri ujenzi wa Soko Kuu linalojengwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Waziri Jafo ametoa pongezi hizo jana Febr. 23 alipotembelea Ujenzi wa miradi mbalimbali Mkoani humo ikiwa ni pamoja na miundombinu inayojengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mvomero, jengo la akina mama na baadae kutembelea ujenzi wa Soko Kuu linalojengwa mjini Morogoro.
Waziri Jafo alionesha kuridhika na kasi pamoja na ubora wa ujenzi huo huku akisema kati ya miradi yote ya Kimkakati inayotekelezwa hapa nchini ni mradi wa soko hilo Mkoani Morogoro pekee ndiyo iliyofanya vizuri katika utekelezaji wake hivyo akawapongeza Viongozi wa Mkoa huo wakingozwa na Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Kebwe Stephen Kebwe kwa kusimamia vizuri ujenzi huo.
Amesema, kwa kazi nzuri inayofanywa na Halmashauri hiyo, yuko tayari kupitisha fedha za miradi mingine ya aina hiyo iwapo wataomba. “kwa speed hii inayoendelea sio dhambi watu kama ninyi kuwapa mradi mwingine, sio dhambi” alisisitiza Mhe. Jafo.
Akiwa Wilayani Mvomero pamoja na kupongeza kazi inayoendelea katika ujenzi wa majengo mengine ya Hospitali ya Wilaya hiyo, Waziri Jafo aliwaonya watumishi wote hapa nchini kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe pamoja na kupokea maelekezo yaliyotolewa na Waziri huyo mwenye dhamana ya TAMISEMI, alibainisha siri ya mafanikio ya ujenzi wa soko Kuu la Manispaa ya Morogoro kuwa ni ushirikiano mzuri uliopo baina ya viongozi wa ngazi zote.
Hata hivyo alimueleza Waziri wa TAMISEMI kuwa tayari kuna miradi ambayo imeshaanza kuibuliwa ukiwemo Mradi wa machinjio ambao umeibuliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa lengo hilo la kutaka kujitegemea kimapato.
Kwa upande wake Mstahiki meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga, pamoja na kutoa shukrani kwa Serikali ya Mhe. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha kwa ajili ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo Ujenzi wa vituo vya Afya, bado alimueleza Waziri juu changamoto iliyopo juu jengo la standi Kuu ya mabasi ya Msavu na kuomba ishughulikiwe.
MWISHO
Haki Miliki © 2018 Mkoa wa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa