Serikali imesema itabatilisha umiliki wa mashamba yote ya wawekezaji ambao wameshindwa kuyaendeleza mashamba hayo kama walivyokubaliana na kutafuta wawekezaji wapya wenye nia ya dhati ya kuyaendeleza maeneo hayo.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula September 26, mwaka huu wakati wa ziara yake ya siku mbili Mkoani Morogoro ambapo atatembelea Wilaya za Kilosa na Mvomero kwa lengo la kukagua uendelezwaji wa mashamba yaliyofutwa umiliki wake na yale yaliyoombewa Ridhaa kwa Rais kufutwa Umiliki wake.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilisha siku ya kwanza ya ziara yake Wilayani Kilosa, Naibu Waziri Mabula amesema yapo mashamba ambayo wawekezaji wake wameshindwa kuyaendeleza hivyo kukwamisha azma ya Serikali ya kuelekea uchumi wa viwanda.
“Kuna baadhi ya mashamba ambayo tumeyaona katika ziara hii yemepandwa mimea katika sehemu ya mbele lakini ukiingia katikati ya shamba ni pori tupu, hii inaonesha wawekezaji hawa wameshindwa kuyaendeleza na hivyo maombi ya kuyafuta umiliki wake yalikuwa sahihi kabisa”. Amesema Naibu Waziri Mbaula.
Aidha, Naibu Waziri huyo ameitaka Halmashauri ya Kilosa kutafuta wawekezaji wapya wenye nia ya kuyaendeleza maeneo hayo yaliyofutwa umiliki wake badala ya kugawa viwanja vya makazi pekee ili Serikali kufikia lengo la Uchumi wa Viwanda.
Awali Naibu Waziri Mabula ameonesha kutoridhishwa na taarifa ya maendeleo ya Wilaya hiyo kutokana na baadhi ya Mashamba yaliyoombewa ridhaa ya kufutwa umiliki wake ambayo yametajwa kutojulikana mahali yalipo huku yakiwa yamesajiliwa ikiwemo shamba la Wami Luhindo hali ambayo naibu Waziri alitaka kupata maelezo zaidi kuhusu suala hilo.
Akijibu suala hilo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilosa Bw. Francis Kaunda amesema wanalichukuwa suala hilo kama agizo na watalifanyia kazi ikiwemo kutafuta maelezo ya kina kuhusu maeneo hayo kama ambavyo Naibu Waziri ameagiza.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri ameitaka Halmashauri Kilosa kuipatia vitendea kazi Idara ya Ardhi ya Halmashauri hiyo ili kurahisisha utendaji kazi wake ukiwemo usafiri kwa ajili ya kutembelea maeneo yenye kero mbalimbali za Ardhi kwa kuwa rasilimali hiyo ina Mchango Mkubwa katika Maendeleo ya Sekta zote.
Sambamba na hilo ameitaka Halmashauri hiyo kukamilisha upimaji wa viwanja ambavyo vilishaanza kupimwa na kuviandalia hati badala ya kuanzisha zoezi jingine la upimaji viwanja wakati viwanja takribani 1,359 vya mwanzo Wilayani humo havijakamilika upimaji wake.
Kuhusu suala la Migogoro ya Ardhi katika Wilaya hiyo Naibu Waziri ameipongeza Halmashauri chini ya usimamizi wa Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Kebwe Stephen Kebwe kwa kupunguza migogoro ya Ardhi kwa wananchi wake huku akiwaagiza watendaji wa Hamashauri hiyo kuweka ratiba ya kwenda kwa wananchi kusikiliza na kutatua kero zao mara mbili kwa wiki badala ya kubaki Ofsini kwa wiki nzima.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi pamoja na shukrani zake kwa Naibu Waziri huyo kutembelea Wilayani kwake, amemuomba kuwasaidia kupunguza Ukubwa wa maeneo yanayomilikiwa na watu wachache huku wananchi wengine wakikosa maeneo kwa ajiri ya kufanya shughuri zao za kiuchumi ikiwemo kilimo.
Mgoyi ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa watakao bahatika kupata Ardhi itakayotokana na mashamba yatakayofutiwa umiliki wake kuitumia kwa ajili ya Kilimo na sio kuuza au kukodisha.
Naibu Waziri Angelina Mabula yupo katika Ziara ya siku mbili Mkoani Morogoro katika Wilaya za Kilosa na Mvomero ambapo atakagua maeneo yaliyofutiwa Umiliki wake na yale yaliyoombewa ridhaa ya kufutwa kutokana na wamiliki wake kushindwa kutekeleza mikataba ya uendelezwaji wa mashamba hayo.
MWISHO
Haki Miliki © 2018 Mkoa wa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa