Magufuli ataka mashamba yanayofutwa wapewe wananchi maskini
Na Andrew Chimesela – Morogoro
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Kilosa na Mkoa wa Morogoro kwa jumla kupanga mikakati mathubuti ya kugawa mashamba yanayofutwa na Serikali kwa wananchi maskini ili kukomesha migogoro inayojitokeza Mkoani hapa.
Rais Magufuli ametoa agizo hili Juni 29, 2020 akiwa Wilayani Kilosa wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi Mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) sehemu ya Morogoro hadi Makutupora na ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Rudewa hadi Kilosa yenye urefu wa Km 24.
Akitoa hotuba yake mbele ya maelfu ya wananchi wa kilosa na maeneo jirani, Rais Magufuli amesema sababu kubwa ya migogoro ya ardhi inayojitokeza Mkoani Morogoro inatokana na mashamba makubwa kuchukuliwa na matajiri.
Kwa sababu hiyo pamoja na mashamba 49 aliyokwisha yafuta, bado amemuagiza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kabla ya jumamosi ya wiki hii, kumpelekea taarifa ya mashamba mengine 11 ili ayafute na kuwagawaia wananchi Maskini lengo ikiwa ni kukomesha Migogoro hiyo.
“lakini ninachotaka kifanyike, na hili ni la muhim zaidi, uongozi wa Wilaya ya Kilosa, na uongozi wa Wilaya zote katika Mkoa wa Morogoro, wakae, haya mashamba yaliyofutwa ni lazima tuyagawe bure kwa wananchi maskini” aliagiza Rais Magufuli.
Amesema, imekuwa ni kawaida mashamba hayo yanayofutwa kugawana matajiri badala ya kutoa kwa maskini ambao ndio walengwa na kusababisha migogoro ya ardhi kuendelea kujitokeza Mkoani Morogoro, hivyo ameagiza uwepo usimamizi madhubuti katika ugawaji wa mashamba yote yanayofutwa.
Akizungumzia Mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro ambao umefikia asilimia 82, Rais Magufuli amefurahishwa na ujenzi huo hususan handaki alilolikagua lenye urefu wa zaidi ya Km 1, na kufurahishwa kuwa ujenzi wake umezingatia kiwango na kasi.
Kuhusu ujenzi wa Barabara ya kiwango cha lami ya kutoka Rudewa hadi Kilosa, inayojengwa na Wakandarasi wazawa, Dkt. Magufuli amesema hajaridhiswa na kasi ya ujenzi huo kwa kuwa ni wa kusuasua. Kwa sababu hiyo ametoa kipindi cha mwezi mmoja Wakandarasi hao kubadilika.
Amesema wasipobadilika atawanyang’anya kazi hiyo na kwamba kuanzia sasa Wakandarasi hao waanze kujenga barabara hiyo usiku na mchana. Amesema, wakandarasi wazawa wamekuwa wakilalamika kutopewa zabuni za kujenga barabara na miundombinu mingine lakini haipendezi wanapopewa zabuni hizo hawazitumii ipasavyo.
Katika hatua nyingine Rais Magufuli amemwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Isack Kamwelwe kuanza kufanya Upembuzi yakinifu wa barabara ya kutoka Kilosa Mjini kwenda Mikumi (Km 78) ili itafutiwe fedha na kujengwa kwa kiwango cha lami.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.