RAS MOROGORO ATOA MWEZI MMOJA MALINYI KUPATA MAJI
Na Andrew Chimesela – Morogoro
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo ameagiza Wakala wa Usamabazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini - RUWASA Mkoani humo, kuhakikisha wananchi wa Malinyi wanapata huduma ya maji Safi na Salama ndani ya kipindi kisichozidi mwezi mmoja kuanzia Agosti 25 mwaka huu.
Mhandisi Kalobelo ametoa agizo hilo Agosti 25 mwaka huu, Wakati wa Kikao cha pamoja cha kujadili hatma ya Mradi wa Maji wa Malinyi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofsisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Agizo hilo limekuja baada ya mradi wa Maji wa Malinyi ulioanza kujengwa mwaka 2015 kutokamailika kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa kusanifu Mradi, hivyo maji kushindwa kufika kwenye tenki.
Baada ya changamoto hiyo kujitokeza uongozi wa Mkoa wa Morogoro umeamua kuingilia kati na kuandaa kikao kwa kuwakutanisha Wadau wa Mradi huo ili kutafuta njia mwafaka ya kuwafikishia maji wananchi wa Malinyi.
Pamoja na kutafuta njia za kufanikisha mradi huo, wajumbe walikubaliana kuwa njia sahihi na ya haraka ya kuwapatia maji wananchi wa Malinyi na kuondokana na kero hiyo, ni kuchimba visima virefu. ndipo Mwenyekiti wa kikao hicho, ambaye pia ndiye Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo akatoa agizo.
“Mimi nisema watu wa Malinyi wanahitaji maji, yanatoka wapi is non of their business (sio kazi yao). Kwa hiyo RUWASA kama RUWASA Option hiyo ya kupeleka visima ichukueni walau kwanza watu wapate maji kwa muda mfupi inavyowezekana na ikiwezekana ndani ya mwezi huu wa tisa” aliagiza Mhandisi Kalobelo.
Hata hivyo alieleza kuwa yeye hatengui maelekezo ya Waziri wa Maji aliyoyatoa alipotembelea mradi huo wa kuboresha mradi wa Maji wa Malinyi bali aliwataka waendelee kuyatekeleza kama Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Maji alivyoagiza.
“Maelekezo ya Waziri mimi sitaki kuyatengua. Maelekezo ya Waziri aliyeelekeza kwamba maboresho ya Mradi huu yafanyike yatekelezwe.” Alisisitiza.
Aidha, Mhandisi Kalobelo amemtaka Mkurugenzi wa RUWASA kuwasiliana na watu Bonde ili kuhakiki ubora wa maji ya visima vinavyopedekezwa kuchimbwa ili mara visima vitakapokamilika maji yaingizwe kwenye miundombinu iliyokwishajengwa na wananchi waanze kupata huduma ya maji.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Kalobelo amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro - MORUWASA Mhandisi Tamim Katakweba kuhakikisha kazi ya kuboresha mradi wa awali inaendelea kufanyika na inakwenda sambamba na uchimbaji wa visima ambavyo vinatasaidia kuondoa tatizo la maji kwa haraka.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Morogoro Mhandisi John Msengi ametoa wito kwa wananchi wa Malinyi kuendelee kuwa watulivu kwa kuwa Serikali kupitia uongozi ngazi ya Mkoa umeshatoa agizo kuwafikishia maji ndani ya mwezi mmoja.
Naye Mkandarasi wa Mradi wa Maji Malinyi Kambarage Masato kutoka Kampuni ya Aundacia Investment Ltd amesema amepokea maagizo ya Katibu Tawala wa Mkoa na kuahidi kuyatekeleza kwa wakati kama walivyokubaliana kwenye kikao hicho.
Kikao hicho cha kujadili hatma ya mradi wa maji Malinyi, kilijumuisha Wajumbe wa Menejimenti ya Mkoa wa Morogoro, Meneja wa RUWASA Morogoro, Mkurugenzi wa MORUWASA, Mkandarasi wa Mradi wa Maji wa Malinyi na Mhandisi Mshauri wa Mradi huo.
Mradi wa Maji wa Malinyi ulianza kutekelezwa 26/92015, ambapo ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi sita na baada ya kushindwa kukamilika ukaongezewa muda wa utekelezaji hadi 16/12/2017.
Mradi huu ulikuwa unatekelezwa na Mkandarasi Aundacia Investment Ltd chini ya Mkandarasi Mshauri wa Kampuni ya Interconsult. mradi ukikamilika unategemea kutoa huduma kwa watu zaidi ya elfu 17 wa vijiji vya Malinyi, Kipingo na Makere.
Hadi sasa fedha zilizokwishalipwa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ni shilingi 2.9 Bil. sawa na asilimia 97.78 ya gharama yote ya ujenzi wa mradi huo ambao ni zaidi ya shilingi 3 Bil.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.