Na. Andrew Chimesela - Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amempongeza Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakari Zuber kwa Ofisi yake kuwa chimbuko la mshikamano wa dini zote unaoendelea kushamiri hapa nchini na kuondoa tofauti zilizokuwepo siku za nyuma.
Dkt. Kebwe ametoa pongezi hizo Disemba 28 mwaka huu wakati akitoa salamu za Serikali ngazi ya Mkoa aliposhiriki mazishi ya Sheikh wa Wilaya ya Morogoro Mjini Abdulrahaman Kiswabi (55) aliyefariki Dunia Disemba 27 saa tatu asubuhi nyumbani kwake Mjini Morogoro.
Dkt. Kebwe amesema ushirikiano mzuri, Amani na utulivu ambavyo vipo Mkoani Morogoro chimbuko lake ni Mufti wa Tanzania baada ya kuanzisha kamati ya Amani ambapo sasa kamati hizo zimesambaa karibu nchi nzima ukiwemo Mkoa wa Morogoro kwani kamati hiyo ni moja ya mafanikio ya Amani na Utulivu wa Mkoa.
“mshikamano huu wa dini zote katika nchi yetu, chimbuko lake ni Mufti. Kwa hiyo naomba mfikishie salamu namshukuru sana, kazi hii nzuri ambayo ameifanya, kamati ya Amani ya Dar es Salaam ilianza na sasa imesambaa kote nchini” alisema Dkt. Kebwe.
Dkt Kebwe aliongeza akisema siku hizi hakuna mihadhara ambayo ilikuwa inatokea siku za nyuma, dini moja kukashfu dini nyingine hii inatokana na matunda ya kazi nzuri ambayo Mufti ameifanya pamoja na timu yake.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kebwe amesema Sheikh Abdulrahaman Kiswabi aliishi vizuri na watu na kutoa wito kwa watu wengine kumuenzi marehemu kwa kuyaishi mema aliyoyatenda marehemu kipindi cha uhai wake katika kutunza Upendo, Amani na Utulivu mambo ambayo pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa akisisitiza mara zote.
Naye Kiongozi wa ULAMAA ambaye pia ni Msemaji wa Mufti hapa nchini Sheikh Hassan Chizenga ambaye alishiriki katika mazishi hayo alisifu ushirikiano uliopo baina ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Serikali kwa jumla na madhehebu ya Dini na kutaka ushirikiano huo udumishwe.
“Kitendo cha Mkuu wa Mkoa na Meya na wote kuhudhuria mazishi haya, kinaonesha kwamba Serikali inatambua mchango wa Viongozi wa Dini katika kujenga Amani na maendeleo ya nchi yetu” alisema Sheikh Chizenga.
Kiongozi huyo wa kidini pia aliwataka waombolezaji waliofika katika msiba huo kuishi kulingana na maelekezo ya mwenyezi Mungu kama alivyofanya Sheikh Abdulrahaman Kiswabi.
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Pascal Kihanga kwa niaba ya wananchi wa Manispaa hiyo, aliwaasa wananchi kuishi vizuri huku akisema kifo kiliumbwa na hakuna haja ya kuhoji kwanini kipo badala yake kila mmoja aishi vizuri kulingana na imani ya dini yake.
Nao waombolezaji waliofika kushiriki mazishi hayo wamemuelezea marehemu kuwa alikuwa na moyo wa kuwapenda watu, alipenda dini yake, alipenda kujifunza na alijituma wakati wote kutumikia dini yake.
Marehemu Sheikh Abdulrahaman Kiswabi amezikwa Disemba 28 kijijini kwao Kikundi (Kilungule) katika Wilaya ya Morogoro Vijijini.
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.