RC Morogoro apokea michango, awashukuru Wadau na kuwaasa.
Na. Andrew Chimesela, Morogoro.
Wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo wafanyabiashara Mkoani Morogoro wameanza kutekeleza ahadi zao za kutoa michango ya fedha na vifaa ili kusaidia kupambana na ugonjwa wa CORONA kama walivyoahidi Aprili 21 mwaka huu waliposhiriki kikao cha kujadili namna ya kupambana na ugonjwa huo Mkoani humo.
Wadau hao wameanza kutekeleza ahadi hiyo leo Aprili 24 kama walivyoahidi mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare siku ya kikao cha Aprili 21 mwaka huu na leo baadhi ya wadau hao wamefika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kutoa fedha na vifaa mbalimbali vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi 140Mil.
Mmoja wa wadau kutoka Islamic Foundation akikabidhi mchango wake kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro. Katikati anayeshuhudia ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo
Baadhi tu ya wadau wa maendeleo wakiwasilisha michango yao Kwa Mkuu wa Mkoa
Akiongea wakati wa tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare amewashukuru wadau wote walioamua kutoa michango yao ya fedha na vifaakinga mbalimbali kwa lengo la kusaidia juhudi za Mkuu huyo wa Mkoa na Serikali kwa ujumla katika kupambana na ugonjwa wa CORONA Mkoani humo.
Aidha, Loata Sanare amewahakikishia wadau waliotoa michango kuwa uadilifu mkubwa utazingatiwa katika kutumia fedha na vifaa vyote vilivyochangwa na vitakavyoendelea kuchangwa na kwamba vitatumika kama ilivyokusudiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare akimkabidhi Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Kusilye Ukio moja ya vifaa vilivyotolewa na wadau kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa CORONA. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Regina Chonjo
Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wadau hao kutoa elimu kuhusu janga la ugonjwa wa CORONA kwa watu wanaowahudumia katika maeneo yao ya kazi au biashara zao na kuhakikisha wanawakinga na janga la ugonjwa huo.
“Na kikubwa sio fedha, kikubwa sio vifaa ambavyo mmevileta hapa, kikubwa ni kutoa elimu hii kwa watu ambo tunawahudumia” ameshauri Sanare
Lori la mizigo likiwa limebeba vifaa mbalimbali vya kusaidia kupambana na maambukizi ya virusi vya COVID - 19 vilivyotolewa na wadau mbalimbali Mkoani Morogoro
Tukio la kupokea michango hiyo ambalo ni la ahamu ya kwanza linalotarajiwa kuendelea kufanyika hapo kesho lilitanguliwa na ziara fupi ya Mkuu huyo wa Mkoa akiambatana na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na kutembelea kiwanda cha kushona nguo za michezo cha Mazava na kiwanda cha kutengeneza nguo cha 21st Centuary .
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa amewataka wamiliki wa viwanda hivyo kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa CORONA kwa kufuata maagizo yanayotolewa na Serikali na Wataalamu wa Afya ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wote kunawa maji tiririka kwa sabuni kila wanapoingia na kutoka kazini pamoja na kuwapima joto lao mara kwa mara ili kuepukana na maambukizi ya Virusi vya COVID - 19.
Mhe. Loata Sanare (katikati) na katibu Tawala wa Mkoa Mhandisi Emmanuel Kalobelo (kulia) wakiwa ghorofani wakiangalia wafanyakazi wa Kiwanda cha Mazava wakiwa kazini mara Mkuu wa Mkoa alipotembelea kiwanda hicho kilichopo katika Manispaa ya morogoro. Kushoto ni Meneja Uzalishaji wa kiwanda hicho Bw. Nelson Mchukye.
Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo alibainisha lengo la ziara ya Mkuu wa Mkoa kuwa ni kutaka kujionea uwezo wa Viwanda hivyo kama vinaweza kuzalisha kwa ubora unaohitajika vifaa vya aina yoyote vya kupambana na ugonjwa wa CORONA kama Barakoa, lengo ni kutekeleza agizo la Rais John Pombe Magufuli la kutengeneza vifaa hivyo hapa nchini.
Meneja Uzalishaji wa Kiwanda cha nguo cha Mazava Bw. Nelson Mchukya akimuonesha Mkuu wa Mkoa barakoa ambazo zimeanza kuzalishwa katika kiwanda hicho, ambapo Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Ukio (mbele kushoto) kufuatilia barakoa hizo kama zina ubora unaostahili ili zitumike.
Kwa upande wao wadau waliofika kutoa michango, waliendelea kutoa ushauri kwa Serikali kuendelea kutoa elimu kwa jamii kujiepusha na mikusanyiko isiyo ya lazima lakini pia wakatoa wito kwa kila mmoja kwa Imani yake kumrudia Mungu wake ili kuliepusha taifa na janga hili hatari.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.