Na. Andrew Chimesela, Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare amesitisha matumizi ya bweni la wavulana la shule ya msingi ya Berhnad Bendel iliyopo Manispaa ya Morogoro kutokana na jengo hilo kukosa sifa ya kutumika kama bweni huku likihatarisha afya za wanafunzi.
Sanare amechukua uamuzi huo Novemba 11 mwaka huu alipotembelea shule hiyo iliyopo eneo la Kola na kushuhudia mazingira mabovu ya jengo hilo linalotumiwa na wanafunzi zaidi ya 100 ambapo aina ya ujenzi wake ukionekana kukosa sifa ya kutumika kama bweni huku likijengwa pasipo kufuata utaratibu wa ujenzi wa matumizi yenyewe.
Mazingira ya bweni hilo yalioneka kutopitisha hewa ya kutosha ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi wanaotumia huku ndani ya jengo kukitawaliwa na harufu kali inayotoka katika vyoo ambavyo vipo ndani ya jengo hilo.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ameagiza kusitishwa mara moja matumizi ya bweni hilo na kutaka wanafunzi hao watafutiwe sehemu nyingine iliyo salama watakayoitumia kama bweni mpaka hapo jengo hilo litakapofanyiwa marekebisho.
“kutokana na hali tuliyoiona wenyewe kwenye jengo lile, nasitisha kuanzia sasa lisitumike tena na muwatafutie sehemu nyingine salama wanafunzi hawa, lakini muhakikishe jengo hilo linajengwa upya ndani ya mwaka huu kwa kufuata utaratibu wa ujenzi wa bweni”, Alisema Sanare.
Hata baada kukosekana taarifa za ujenzi wa bweni hilo na uhalali wa matumizi yake kama bweni Mkuu wa Mkoa Sanare amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro Janeth Machulya kufuatilia taarifa ya ujenzi wa jengo hilo.
Sambamba na hayo Mkuu wa Mkoa amemtaka Afisa Afya Mkoa wa Morogoro kuchukua hatua za kisheria kwa shule hiyo kufuatia kuwepo kwa mifereji ya maji taka inayotiririka kwenye maeneo yasiyo sahihi na kuhatarisha afya za wanafunzi.
Kuhusu ukaguzi wa mara kwa mara wa shule, Mkuu wa Mkoa amemtaka Mdhibiti ubora wa shule Manispaa ya Morogoro kuhakikisha anafanya zoezi la ukaguzi wa mara kwa mara ili kujiridhisha wakati wote mazingira ya shule yanakuwa safi na salama kwa wanafunzi na watumiaji wengine katika shule hiyo.
Kwa upande wake Kamanda wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro Janeth Machulya amesema Taasisi yake imepokea maagizo ya Mkuu wa Mkoa na atayafanyia kazi mara moja.
Naye Mkuu wa shule hiyo SR. Levina August amekiri kuwepo kwa changamoto zilizoonekana katika ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa ambapo ameahidi kwasiliana na mmiliki wa shule hiyo ili kushughulikia maagizo yote yaliyotolewa na kiongozi huyo.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.