Na. Andrew Chimesela, Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare amesema endapo wafugaji hawatotii kanuni, taratibu na maelekezo ya namna bora ya kufuga mifugo yao ataruhusu kutaifishwa mifugo yote itakayobainika kuingizwa katika mashamba ya wakulima na kuharibu mazao ili kuwa sehemu ya kudhibiti migogoro baina ya wakulima na wafugaji Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa ameyasema Disemba 20, mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Ualimu Morogoro wakati akifungua kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) kinachojadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo.
Sanare amesema mbali na kutaifishwa mifugo kwa upande wa wafugaji watakaokiuka taratibu na maelekezo,wakulima watakaovamia maeneo ya wafugaji mazao yao yataruhusiwa kulishia mifugo.
Aidha, Sanare ameziagiza Halmashauri zote za Mkoa huo kuhakikisha Fedha zote za mapato zinazokusanywa katika vyanzo mbalimbali zinawekwa Benki kwa kufuata utaratibu na maelekezo ya Serikali kabla ya matumizi yoyote.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa, ameonesha masikitiko yake kwa baadhi ya wakandarasi wanaoshindwa kukamilisha miradi kwa wakati na wale wanaojenga chini ya kiwango ameagiza wakandarasi wote ambao bado hawajakamilisha miradi yao kulingana na muda waliopewa wakamilishe mara moja.
Sambamba na hayo amewataka wadau wa Elimu katika Halmashauri zote kuhakikisha wanafunzi wote wenye sifa za kujiunga kidato cha kwanza wanaanza masomo yaomuda utakapofika na kuagiza kutolewa vibali kwa shule zilizokidhi vigezo ili zipokee wanafunzi lengo likiwa ni kuhakikisha hakuna mtoto aneyekosa kwenda shule kwa sababu ya upungufu wa vyumba vya madarasa.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.