Viongozi tekelezeni wajibu, Maafisa Biashara tendeni haki – RC Sanare
Na Andrew Chimesela, Ifakara Morogoro
Viongozi mbalimbali wa Serikali Mkoa wa Morogoro wametakiwa kutimiza wajibu wao ipasavyo huku Maafisa Biashara ndani ya Mkoa huo kutakiwa kutenda haki wakati wote wa zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo 2020 ili nia njema ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwajali wanyonge iweze kutimia.
Rai hiyo imetolewa Mei 21 mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare wakati wa Uzinduzi rasmi wa ugawaji wa vitambulisho vya wafanya biashara na watoa huduma wadogo mwaka 2020 uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Wilayani humo.
Loata Sanare amesema zoezi hilo ili mwaka huu litekelezwe kwa ufanisi, ushirikiano thabiti unahitajika kuanzia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi za Wakurugezi Watendaji wa Halmashauri na Maafisa wa TRA huku Wafanyabiashara wakiwa ndio waratibu wakuu.
Katika hatua nyingine Loata Sanare amewaagiza Maafisa Biashara kutenda haki katika ugawaji wa vitambulisho hivyo huku akiwataka viongozi wengine wa Serikali kutorudia changamoto zilizojitokeza mwaka 2019.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuzindua zoezi hilo la kugawa vitambulisho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo alibainisha faida ya vitambulisho hivyo kuwa vinawawezesha wafanya biashara na watoa huduma wadogo wa sekta isiyo rasmi kufanya biashara zao bila kubughudhiwa.
Hata hivyo alibainisha changamoto zilizojitokeza mwaka jana kuwa ni pamoja na kutohifadhi kumbukumbu sahihi ya orodha ya majina ya wafanyabiashara na watoahuduma hao.
Changamoto ya pili ni wahusika wa kugawa vitambulisho hivyo kukaa na fedha mikononi mwao badala ya kupeleka Benki hivyo kuchelewesha uwasilishaji wa fedha hizo kwa wakati kwenye mamlaka husika huku utoaji wa Elimu juu ya faida ya vitambulisho haukufanyika ipasavyo ikiwa ni changamoto iliyofanya vitambulisho hivyo kutochukuliwa kwa wingi.
Mkoa wa Morogoro kwa mwaka huu 2020, utapewa jumla ya vitambulisho 60,000 kwa mwaka mzima. Mkoa umekwishapokea jumla ya vitambulisho 12,000 ikiwa ni awamu ya kwanza na awamu ya pili Mkoa utaletewa Vitambulisho 48,000.
Baada ya Mkuu wa Mkoa kuzindua rasmi zoezi hilo la ugawaji wa Vitambulisho aliwakabidhi Wakuu wa Wilaya zote saba na kutakiwa kuanza kuvigawa mara moja ambapo Wilaya ya Kilosa imepata vitambulisho 2000, Ulanga 750, Gairo 900, Malinyi 620, Morogoro 3930, Mvomro 2000, na Kilombero vitambulisho1800.
Vitambulisho hivyo vitagawanywa kwa wale wafanyabiashara waliokidhi vigezo ikiwa ni pamoja na wale wenye biashara zao ambazo mauzo yake hayazidi Shilingi milioni Nne kwa mwaka na sio wenye mitaji isiozidi shilingi milioni Nne kwa mwaka.
Sharti jingine wafanyabiashara watakaopata vitambulisho hivyo ni wale ambao hawajawahi sajiliwa na TRA na kuwa na TIN namba.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.