RC Sanare awanga’ang’ania wafanyabiashara wakubwa wa Sukari
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare ameendelea kuwang’ang’ania wafanya biashara wa maduka ya jumla Mkoani humo kuuza sukari wanayoletewa kwa kufuata bei elekezi ya Serikali kama walivyokubaliana wakati wa kikao kati yake na wafanyabiashara hao.
Loata Ole Sanare ametoa kauli hiyo Mei 13 mwaka huu alipofanya ziara ya kushtukiza ya kutembelea baadhi ya wafanyabiashara wa maduka hayo ili kujionea uhalisia wa kuuza suakari unavyofanyika katika Manispaa ya Morogoro.
Akiongozana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa Mkuu huyo wa Mkoa bado amebaina baadhi yao wafanyabiashara hao wameendelea kuuza Bidhaa hiyo zaidi ya bei elekezi ya shilingi 127, 000 kwa mfuko mmoja wa sukari wa kilogramu 50 hivyo kukiuka maagizo ya Serikali.
Sanare amewataka Wafanyabiashara hao kufuata utaratibu na maelekezo ya Serikali ya kuuza sukari hiyo na kuridhika na faida wanayopata ili wauzaji wadogo nao wanapowauzia wananchi wa kawaida waweze kupata faida.
Amesema bila kufanya hivyo wananchi wataendelea kuumia kwa kukosa Sukari ama kupata kwa kuuziwa bei ya juu jambo ambalo yeye hatakubaliana nalo. “fuateni maelekezo, tumekaa na wataalamu wetu hapa wamepiga mahesabu wameona bei elekezi kwa Mkoa wetu wa Morogoro inafaa” alisisitiza Mkuu wa Mkoa.
Ikumbukwe kabla ya ziara hii mei 8 mwaka huu Mkuu wa Mkoa huo alikutana na wafanyabiashara wakubwa wa sukari hapa Mkoani Morogoro na kukubalina kuuza Sukari itakayoletwa kwa bei elekezi ambayo ni shilingi 127,000 kwa kila mfuko mmoja wa sukari wa kilo hamsini.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.