Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare ameagiza kuchukuliwa hatua viongozi wote ngazi ya vijiji, kata hadi tarafa watakaobainika kutowajibika ipasavyo katika utendaji kazi wao na kupelekea kuendelea kuibuka kwa migogoro ya mara kwa mara baina ya jamii ya wafugaji na wakulima katika maeneo yao.
Sanare ameayasema hayo Februari 22 mwaka huu wakati akiongea na viongozi wa vijiji, kata, viongozi wa jamii za wakulima na wafugaji pamoja na wananchi wa tarafa ya Mikese iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji kwa kiasi kikubwa inasababishwa na baadhi ya viongozi wa Serikali kukosa uaminifu wakiwemo wenyeviti wa vijiji na watendaji wa kata na vijiji wanaofanya biashara ya kuuza ardhi kwa wageni pasipo kufuata utaratibu jambo linalopelekea kuibuka kwa migogoro baina ya pande mbili za Jamii ya wakulima na wafugaji kila kukicha.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akiongea na viongozi wa vijiji, kata, tarafa pamoja na viongozi wa wakulima na wafugaji.
Kutokana na hali hiyo Sanare ameweka bayana kuwa hatamvumilia mtendaji yeyote wa Serikali au mwenyekiti wa Kijiji atakayebainika dhahiri kuwa yeye ni sehemu ya kusababisha migogoro katika eneo lake na badala yake atakuchukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani kwa kushindwa kutimiza majukumu yake.
“Tarafa hii ya Mikese ni Tarafa ambayo ina migogoro mingi ya Ardhi, tulichojifunza hapa ni kwamba migogoro hii ya ardhi inasababishwa na mambo mengi ikiwemo viongozi wa vijiji na kata ambao wanaingiza watu kutoka maeneo mengine pasipo kufuata utaratibu na kupelekea migogoro”, alisema Sanare.
Akiwa katika mkutano huo, Loata Sanare alielezwa na wananchi kwamba jeshi la polisi limekosa uaminifu kwa kile kilichoelezwa kwamba limekuwa likitumiwa vibaya na baadhi ya watu ili kutetea maslahi yao binafsi na kushindwa kutenda haki kulingana maadili na majukumu ya jeshi hilo.
wananchi wa tarafa ya mikese wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare.
Kufuatia malalamiko hayo, Sanare amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoani humo kufuatilia malalamiko hayo na kuhakikisha haki inatendeka, kwani jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kusimamia sheria na sio maslahi ya mtu mmojammoja.
Aidha, Sanare amezitaka jamii za wakulima na wafugaji katika maeneo hayo kuishi kwa kuheshimiana kwani ni wazi kwamba jamii zote zinaishi kwa kutemegemeana hivyo hakuna sababu ya kugombana huku akisisitiza kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa wale watakaoonekana kuwa wakorofi na kuwa sababu ya migogoro ndani ya maeneo wanayoishi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Rehema Bwasi.
Ameongeza kuwa Serikali Mkoani humo itaendelea na msimamo wake wa kutaifisha nusu ya mifugo ya mfugaji atakayelisha kwenye shamba la mkulima ikiwa ni pamoja na kumchukulia hatua za kisheria mmiliki wa mifugo hiyo huku hatua kali pia zikichukuliwa kwa mkulima atakayevamia eneo la mfugaji na kugeuza kuwa eneo la kilimo ikiwemo mazao yake yote kulishiwa mifugo na mwenyewe kuchukuliwa hatua za kisheria.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ameuagiza Uongozi wa tarafa ya Mikese kuwaandikia barua ya wito wamiliki wa minara ya simu ya kampuni za mawasiliano ya Vodacom na Tigo iliyopo katika eneo la Mikese kufika na kueleza sababu ya kutolipa kodi ya minara yao kwa kijiji husika na ikithibitika hawajalipa basi watatakiwa kulipa malipo hayo tangu waliposimika minara yao kwani suala hilo limekuwa ni moja ya kero kijijini hapo.
mwananchi wa tarafa ya mikese akitoa kero yake mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bi. Regina Chonjo amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Rehema Bwasi kuwasimamia ipasavyo wakuu wake wa Idara ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwani wao wanaweza kuwa wanachangia kawa kiasi kikubwa kukwama kwa baadhi ya mambo mbalimbali na kupelekea kuibuka migogoro katika jamii.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Regina Chonjo.
Mkuu wa Mkoa huyo alifika Katika Tarafa ya Mikese kufuatia Uongozi wa kijiji cha Mikese kilichopo tarafa ya Mikese Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kumwandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare ukimuomba kufika Kijijini kwao ili kusaidia kutatua kero mbalimbali zilizopo katika Kijiji hicho na vijiji jirani vya Tarafa ya Mikese ikiwemo migogoro ya wakulima na wafugaji, uwepo wa mashamba pori na kutolipa Kodi minara ya makampuni ya simu ya Vodacom na Tigo iliyosimikwa tangu mwaka 2002.
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.