Skauti Morogoro wampongeza Magufuli, watoa wito kwa jamii.
Na Andrew Chimesela – Morogoro
Chama cha Skauti Mkoani Morogoro kimempongeza Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuwa mzalendo namba moja na kuinua Uchumi wa watanzania.
Pongezi hizo zimetolewa hivi karibuni na Kamishina Mstaafu wa Skauti Mkoa wa Morogoro Francis Gaspal Francis wakati walipotembelea shule ya Msingi Buigiri iliyopo Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma yenye wanafunzi wenye uoni hafifu na wenye ulemavu wa ngozi kwa ajili ya kutoa misaada mbalimbali katika shule hiyo.
Kamishina Francis Gaspal amesema, Skauti inafanya kazi bega kwa bega na Serikali katika kuwasaidia watu waliopatwa na majanga mbalimbali na kuwajali wanyonge jambo ambalo Serikali ya awamu ya tano inalifanya kwa vitendo, kwa sababu hiyo wamempongeza na kwamba wanaunga mkono jitihada hizo za Rais Magufuli.
“Rais John Pombe Joseph Magufuli amejitahidi sana katika kuinua uchumi wetu wa Tanzania kwa hiyo sisi kama Skauti tunaunga mkono matukio yote anayoyafanya Rais wetu katika kuhakikisha Uchumi wa Tanzania unaenda mbele” alisema Kamishna Francis.
Kamishina Francis amebainisha kuwa Skauti ni chama cha kufanya kazi za kujitolea zaidi kwa lengo la kutekeleza moja ya ahadi kuu za chama hicho ya kuwa Mzalendo wa kweli kwa nchi yao na kuwapenda watu wote.
Amezitaja baadhi ya kazi zilizofanywa na Skauti Mkoa wa Morogoro kuwa ni pamoja na ushiriki wao katika kuokoa watu tukio la mafuriko ya Wilayani Kilosa mwaka 2018, kushiriki ujenzi wa daraja la Dumila wakati limekatika 2014, ajali ya moto iliyotokea eneo la Msamvu 2019 Mkoani Morogoro na matukio mengine mengi.
Katika hatua nyingine Kamishina huyo Mstaafu ametoa wito kwa jamii kuthamini jitihada zinazofanywa na chama cha Skauti Tanzania za kuwaokoa watu wakati wa majanga lakini pia ameitaka jamii itoe ushirikiano kwa Skauti wanapokuwa wanafanya kazi zao ili watekeleze azma yao ya kuokoa waliofikwa na majanga.
Naye Mlezi wa Vijana wa Skauti Walioshiriki kutembea kwa miguu kutoka Morogoro Mjini hadi Dodoma Mjini Bi. Zainabu Ayub pamoja na kumpongeza Dkt. John Pombe Magufuli kwa uongozi wake thabiti amesema shughuli za Skauti zinamuimalisha mtu kimwili muda wote na kumfanya kuwa imara kiakili.
Mkuu wa shule ya Msingi Buigiri inayojumuisha watoto wenye uoni hafifu na watoto wenye ulemavu wa ngozi Samweli Jonathan pamoja na kushukuru zawadi zilizotolewa na Skauti hao aliomba ushirikiano ulioanzishwa baina ya pande hizo mbili udumishwe kwa manufaa ya pande hizo.
Aidha, Mlezi wa vijana wa Skauti wa shule hiyo John Peter Tongoo ambaye ana uoni hafifu ameomba vifaa mbalimbali kwa ajili ya chama cha Skauti kilichopo shuleni hapo ili chama hicho kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na kuwa Bora zaidi.
Naye mwanafunzia Daniel Eliabi kwa niaba ya wanafunzi wenzake wa shule hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika ametaja changamoto zinazoikabili shule yao kuwa ni pamoja na uchache wa Vitabu vya kufundishia shuleni hapo na kuomba kujengewa uzio wa shule, ili kusaidia Ulinzi na Usalama wao.
Viongozi hao wa Skauti Mkoa wa Morogoro wamefanya ziara ya siku moja katika shule hiyo, kukumbuka fadhila waliyofanyiwa na shule hiyo mwaka 2017 walipopewa malazi hapo shuleni wakati Skauti hao walipotembea kwa Miguu kutoka Morogoro hadi Dodoma kwa ajili ya kuadhimisha miaka 100 ya kuanzishwa kwa chama cha Skauti hapa nchini.
Pamoja na kuadhimisha miaka 100 ya Skauti Tanzania tangu kuazishwa kwake mwaka 2017, matembezi hayo yalibeba ujumbe mahususi kwa jamii ikiwa ni pamoja na kupiga vita mimba za utotoni na utunzaji wa mazaingira.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kamishina Francis Gaspal, Mlezi wa Skauti hapa nchini ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Skauti ni Waziri wa Elimu wa Tanzania na Skauti Mkuu wa Tanzania ambaye huteuliwa na Mlezi wa Skauti ni Bi Mwantumu Mahiza ambaye ni Mkuu wa Mkoa Mstaafu.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.