TFRA YAHAMASISHA MFUMO WA UNUNUZI WA MBOLEA WA PAMOJA.
Mawakala wa kusambaza pembejeo za kilimo Mkoani Morogoro wametakiwa kuwa wavumilivu katika kuutekeleza mfumo mpya wa ununuzi wa pembejeo za kilimo unaowataka mawakala hao kununu pembejo hizo kwa pamoja wakati soko la pembejeo duniani linapokuwa chini.
Hayo yameelezwa na Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji mali Mkoa wa Morogoro Bw. Ernest Mkongo wakati akifungua Semina ya mafunzo ya siku moja kwa mawakala wa kusambaza pembejeo na wataalamu wa kilimo semina iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Aprili 12 mwaka huu.
Bw. Mkongo amesema kila lenye mwanzo halikosi changamoto hivyo ni jukumu la mawakala hao kuwa wavumilivu wanapokutana na changamoto zozote katika mfumo huu mpya ambao lengo lake ni kutaka kunufaisha Mawakala, Serikali na Wananchi kwa ujumla.
“Mfumo huu ndugu zangu ni mfumo mpya na kama tunavyo jua kitu kipya kinapoanza kinakuwa na changamoto zake”. Alisema Bw. Mkongo.
Katika kikao hicho, mtaalam wa elimu ya jamii kutoka TFRA Bi. Rose Mdezi alisema kuwa mfumo wa BPS (Back procurement system) ambao unahusu ununuzi wa pamoja wa mbolea una lengo la likiwa ni kuhakikisha mbolea inanunuliwa kwa pamoja wakati bei ya mbolea katika soko la dunia ni ndogo ili itakapofika nchini mkulima aweze kuipata kwa bei ya chini.
‘’Lengo letu kubwa sisi kama TFRA ni kuhakikisha wakulima wanapata mbolea kwa bei wanayoweza kuimudu’’ alisema Bi. Rose.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mawakala wa kusambaza mbolea Mkoa wa Morogoro Michael Mpembwa alisema mpango huu ulio letwa na TFRA unaenda kutatua changamoto za mbolea ambazo wasambazaji wanakutana nazo. Alisema, awali Serikali haikuwa karibu na mawakala kutokana na kutoshughulikia changamotowalizo kuwa wakikabiliana nazo lakini kwa sasa kupitia huu utaratibu watakuwa na ukaribu zaidi.
Naye Veronika Komba ambae pia ni wakala wa mbolea alisema changamoto kubwa wanazokutana nazo licha ya serikali kuja na mpango huo ambao unaweza kusaidia kusambaza mbolea kwa ufanisi ni Serikali kutolipa madeni yao kwa wakati na hivyo kusimamisha biashara zao na suala la bei elekezi ya pembejeo ambayo imepangwa bila kuzingatia umbali au utofauti wa mahali pembejeo inakopelekwa.
Kwa upande wake Afisa kilimo wa Mkoa wa Morogoro Dk. Rozaria Rwegasila alisema mafunzo haya ya TFRA yatasaidia pande zote mbili kwa upande wa serikali na mawakala kwa kuwa elimu iliyotolewa inaelekeza mawakala namna ya kutatua changamoto walizonazo. Kuhusu madeni yanayodaiwa na mawakala, Dk. Rwegasira amesema Serikali inaendelea na uhakiki wa madeni hayo na mara itakapokamilisha wale wenye madeni halali watalipwa fedha zao.
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.