Na. Andrew Chimesela - Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ameiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Kilombero na Mkoa wa Morogoro kumtafuta na kumkamata mtumishi mmoja wa Halmashauri ya Ifakara Mji kwa tuhuma za kukimbia na fedha za makusanyo ya halmashuri hiyo zaidi ya shilingi million 146.
Loata Sanare ametoa agizo hilo Oktoba 28 mwaka huu wakati wa ziara yake ya kujitambulisha wilayani Kilombero Mkoani humo kutumia fursa hiyo kuongea na watumishi wa Halmashauri ya Mji Ifakara na Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.
Pamoja na kuomba ushirikiano wa kutosha kutoka kwa watumishi wote wa Wilaya ya Kilombero Mkuu huyo ameendelea kufuatilia utekelezaji wa Maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa Majaliwa aliyoyatoa wakati wa Ziara yake aliyoifanya mwezi Septemba mwaka huu Mkoani Morogoro.
Pamoja na kuzitaka Halmashauri zote kutekeleza haraka maagizo yote aliyoyatoa Waziri Mkuu, Sanare ameagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo kumtafuta na kumkamata mtumishi wa halmashauri ya Ifakara Mji Kassimu Chakachaka ambaye anatuhumiwa kutoroka na fedha za Halmashauri hiyo zaidi ya shilingi milioni 146.
Katika hatua nyingine Ole Sanare ameibebesha lawama Kamati ya Fedha ya Madiwani wa Halmashauri hiyo kwa kushindwa kusimamia fedha za Halmashauri hiyo kwa kuwa fedha nyingi zimepotea mikononi mwa watumishi wachache zikiwemo zaidi ya shilingi milioni 210 na nyingine kutumika pasipo kufuata utaratibu wa Kiserikali katika matumizi yake na wao kushindwa kuchukua hatua stahiki.
Pia Mkuu huyo wa Mkoa amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero na Ifakara Mji kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote waliosimamishwa kazi kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha za serikali.
Naye Mtendaji Mkuu wa shughuli za Serikali Mkoa wa Morogoro ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo amewataka watumishi wote wa Halmashauri ya Kilombero na Ifakara Mji pamoja na Mkoa mzima kuzingatia maadili katika utendaji wao wa kazi, Uzalendo na kutimiza majukumu yao kwa wakati.
Loata Ole sanare kwa kutembelea halmashauri hizo sasa atakuwa amebakiza Halmashauri mbili za Ulanga na Malinyi kukamilisha ziara yake ya kujitambulisha kwa halmashauri zote tisa katika Mkoa huo huku akipitia baadhi ya miradi kuona utekelezaji wake.
MWIISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.