“Tusome pamoja” inavyoinua kiwango cha Elimu Morogoro
Na. ndrew Chimesela - Morogoro
Imeelezwa kuwa mradi wa TUSOME PAMOJA unaotekelezwa Mkoani Morogoro umekuwa ni chachu katika kuinua kiwango cha Elimu Mkoani humo hususan katika shule za Msingi baada ya mradi huo kutumia dhana shirikishi katika utekelezaji wake.
Mafanikio hayo yameelezwa Mei 28 mwaka huu na Mwezeshaji wa Ushiriki Jamii wa Programu hiyo ya Tusome Pamoja Mkoa wa Morogoro Bw. Raphael Kibindo wakati wa ziara ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa Programu hiyo katika Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.
Mwezeshaji Raphael amesema sio kwamba Tusome Pamoja umemaliza kutatua changamoto za Sekta ya Elimu Mkoani humo lakini amesema mradi umeondoa kwa kiasi fulani tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali Katika Sekta ya Elimu ya kufanya kazi kwa mazoea hususan walimu katika shule za Msingi na kwa sasa walimu wanatumia mbinu zilizoelekezwa na Mradi katika kuwafanya wanafunzi waelewe “K” tatu yaani Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.
“kwenye kila eneo imekuwa ikifanya kazi vizuri, utaona walimu wana stadi nzuri za kufundisha za kumfanya mtoto aweze kujifunza vizuri kusoma, kuandika na kuhesabu” alisema Bw. Raphael.
Aidha, Mwezeshaji Raphael ametoa Wito kwa Serikali hususan kwa Watendaji ngazi ya Wilaya na Kata kufanya ufuatiliaji katika kutekeleza azma ya Mradi huo kwa kufanya vikao vya mara kwa mara ili kujikumbusha majukumu yao na kutatua changamoto zinazojitokeza, lengo ni mwanafunzi aelewe K tatu huku akiwataka Wazazi kwa kila shule kuona kuwa shule wanazosoma watoto wao ni mali yao.
Naye Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Mhandisi Joyce Baravuga katika ziara hiyo baada ya ufuatiliaji huo na kufanya mahojiano na Walimu Wakuu wa shule za Msingi na Waratibu Elimu wa Kata za Magomeni na Mkwatani Wilayani humo pamoja na changamoto zilizopo amekiri kuwa mradi huo ni chachu katika Elimu Wilayani Kilosa.
Hata hivyo, Mhandisi Baravuga amehoji sababu ya zaidi ya shule 31 za Wilaya hiyo kutoingiza takwimu za shule zao kupitia Vishikwambi (Tablets) ambazo zimetolewa na Mradi wa tusome pamoja na kuziwasilisha ngazi za juu kwa kutumia Vishikwambi hivyo na kusababisha Wilaya ya kilosa kuwa nyuma katika utekelezaji wa Programu ya Tusome Pamoja.
Kwa sbabu hiyo, Mhandisi Baravuga ametoa mwezi mmoja kwa Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Kilosa Mwl. Christina Hauli kuwasimamia Waratibu Elimu Kata kuhakikisha kuwa ifikapo Juni 30 mwaka huu shule zote 158 za Wilaya ya Kilosa ziwe zimeingiza takwimu husika kupitia vishikwambi vyao vinginevyo hatua za kinidhamu zichukuliwa dhidi yao.
Mwezeshaji wa Ushiriki Jamii wa Programu ya Tusome Pamoja Mkoa wa Morogoro Bw. Raphael Kibindo (kulia)akitoa akitoa maelekezo kwa wajumbe wa kikao wakati wa ufuatiliaji wa utekelezaji wa program hiyo Wilayani Kilosa.
Kwa upande wao Waratibu Elimu Kata na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi akiwemo Mwl. Mkuu Erick Yusuph wa shule ya Msingi Lamulilo Kata ya Magomeni Wilayani humo pamoja na kupokea maagizo ya Afisa Elimu Mkoa wanakiri kuwa Programu ya TUSOME PAMOJA imewaleta pamoja baina yao na wadau wengine wa Elimu wakiwemo Umoja wa Wazazi – UWAWA.
Mwl. Yusuph ametaja maeneo ambayo UWAWA wameonesha ushirikiano kwa vitendo kuwa ni pamoja na suala zima la utoaji wa chakula kwa wanafunzi wa darasa la Saba na darasa la awali hali iliyoongeza mahudhurio shuleni na kupunguza idadi ya wanafunzi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu katika shule zao.
Mradi wa TUSOME PAMOJA hapa nchini umeanza tangu mwaka 2016 na unatekelezwa Mikoa yote ya Zanzibar na Mikoa minne (4) ya Tanzania bara ambayo ni Iringa, Ruvuma Mtwara na Morogoro ukiwa na lengo la kuongeza na kuinua stadi za ufundishaji wa KKK kwa wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili ili wajue vema kusoma, kuandika na kuhesabu.
Mradi huu unatekelezwa kwa ufadhiri kutoka Marekani (US AID) na unatarajiwa kuisha mwaka 2021.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.