Dkt. Kebwe asisitiza Ujenzi Miradi ya maendeleo kufanywa usiku na mchana
Na. Andrew Chimesela – Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe ameendelea na msimamo wake kwa kuwaagiza waandamizi wake Mkoani humo kuendelea kutekeleza usiku na mchana ujenzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa Mkoani humo.
Dkt. Kebwe ameonesha msimamo huo na kutoa maagizo hayo wakati wa ziara yake aliyoifanya mwishoni mwa wiki ambapo alitembelea Wilaya za Ulanga na Malinyi kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya hizo.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na Ujenzi wa Vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari ya Iragua (Ulanga), Hospitali ya Wilaya ya Malinyi, Vituo vya Afya vya Ngohelanga (Malinyi) na wakati akirejea kutoka katika ziara hiyo alikagua kituo cha Afya cha Mikumi kilichopo katika Wilaya ya Kilosa.
Miradi yote hiyo aliyotembelea alisisitiza ujenzi kufanyika usiku na mchana ili kwenda na wakati ingawa tayari baadhi ya miradi iko nyuma ya wakati lengo wananchi waweze kupata huduma zinazohitajika kupitia vituo hivyo huku akiwataka watendaji wa Halmashauri hizo kuanza kuandaa utaratibu wa kuwapata haraka wahudumia watakaohudumia vituo hivyo.
Wakati wa ziara hiyo pia Mkuu wa Mkoa huyo kupitia mikutano ya wananchi alihamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa Afya iliyoboreshwa – CHF ili mifuko hiyo iweze kuwasaidia kupata matibabu hata pale ambapo wamepatwa na maradhi lakini hawana fedha taslimu.
“ugonjwa hauna adabu, haupigi hodi wakati unakuja unaweza kuugua hata wakati hauna fedha, hivyo ni vema wananchi kujiunga na Mfuko huu wa Afya wa CHF ili uwe salama utakaokuwezesha kupata tiba hata kama huna fedha mkononi” alisema Dkt. Kebwe.
Katika hatua nyingine Dkt. Kebwe alimuagiza kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Tarimo kuratibu kikao cha pamoja baina ya Uongozi wa Mkoa na Wamiliki wa Hospitali binafsi zikiwemo za Lugala (Malinyi), St. Kizito (Kilosa), Bwagala (Mvomero) na nyingine ili kuona namna hospitali hizo kuweza kutoa huduma za Afya kwa wananchi wenye kadi za CHF.
Hii inatokana na kubainika kwa baadhi ya Hospitali hizo kutokubali kutoa tiba kwa wananchi kupitia mfuko wa CHF kwa sababu mbalimbali ikiwemo ile inayodaiwa kuwa ni ucheleweshwaji wa malipo kwa Hospitali hizo kutoka Serikalini.
CHF iliyoboreshwa kwa sasa inapokea wananchama kuanzia mmoja hadi sita kwa malipo ya shilingi thelathini tu kwa mwaka na kutibiwa bure kwa kipindi hicho popote atakapokuwa, hii ni sawa na mtu mmoja kulipa shilingi elfu tano tu kwa kupata matibabu ya mwaka mzima.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.