Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amewataka Wataalamu wa Mifugo kufanyia kazi Elimu na ujuzi wanaoupata katika Mafunzo mbalimbali kwenye vikaokazi ili kuwasaidia wafugaji kufuga kisasa na kuboresha uchumi wao.
Mhandisi Kalobelo ametoa wito huo katika Kikao cha Mafunzo kwa Wakaguzi wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula na Mifugo kilichofanyika Oktoba 22 mwaka huu katika Ukumbi wa Engineering Bioprocessing uliopo SUA Mkoani Morogoro.
amesema wizara ya Mifugo na Uvuvi imeandaa mafunzo hayo kwa wataalamu hao kwa lengo maalumu ili watakaporejea katika maeneo yao waweze kuwasaidia wafugaji kutambua kuwa kufuga ni Uchumi.
Amebainisha mbele ya wajumbe wa kikao hicho kuwa imekuwa ni kawaida kwa watumishi waliowengi wanaoshiriki mafunzo kutoonesha elimu au ujuzi wanaopata kwenye mafunzo kwenye vikao kazi, hivyo kunakuwa hakuna tofauti kati ya mtumishi aliyepata mafunzo na ambaye hakupata mafunzo, badala yake anaendelea na utaratibu wake wa kila siku (business as ussually).
Sambamba na agizo hilo Kalobelo amewataka Wakaguzi hao mara tu baada ya kumaliza Mafunzo kuandika ripoti ya mafunzo hayo na kuonesha namna watakavyotoa Elimu hiyo kwa wafugaji katika kuwezesha wazalishaji na wafugaji wa Vyakula vya Mifugo kuendelea kufuga kisasa zaidi.
Aidha, Kalobelo amewataka Wakaguzi kufanya kazi zao kwa kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu ili kulinda afya ya Walaji na Mifugo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya kutosha kwa wadau waliopo kwenye mnyororo wa thamani kwenye Tasnia ya vyakula vya mifugo, kufanya hivyo kutatatua changamoto ya matumizi ya Vyakula na rasilimali za vyakula vya mifugo visivyo na ubora hapa nchini.
“Mafunzo haya yawe chachu kwenu na kwa kuwasaidia wafugaji kuzalisha mifugo kwa tija kwa kutumia vyakula kutoka maeneo yaliyosajiliwa na kutambulika kisheria hatimaye kuongeza mchango wa Sekta ya Mifugo katika kuinua uchumi ngazi ya kaya na pato la nchi kwa ujumla”
Mafunzo ya Wakaguzi wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo yanatolewa ili kuwezesha kutatua changamoto za ubora na viwango hafifu vya vyakula vya mifugo vinavyotumiwa na wafugaji wengi kwani kumeonesha zipo athari za ukuaji hafifu kweye kuku,mbwa ,nguruwe na sungura.
Kikao hicho kilishirikisha wakaguzi wa maeneo ya malisho na Rasilimali za vyakula vya mifugo kutoka maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na wataalamu kutoka ngazi ya Mkoa, Wilaya na Serikali za Mitaa.
MWISHO.
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.