Na Andrew Chimesela - Morogoro.
Watoto wapatao milioni 8,082, 838 wenye umri chini ya miezi tisa hadi umri wa miaka mitano Wanatarajia kupata chanjo ya Surua na Rbella na wengine milioni 4, 041, 934 wenye umri wa mwaka mmoja na nusu watapatiwa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa kupooza (Polio).
Hayo yamesemwa Oktoba 17 mwaka huu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati akizindua Kampeni ya chanjo ya Surua, Rubella na Polio kwa mwaka 2019 iliyofanya kitaifa Mkoani hapa.
RC Morogoro akimkaribisha rasmi mgeni wake katikauwanja wa Jamhuri kwa ajili ya kuzindua kampeni ya chanjo.
Aidha, Waziri Ummy Mwalimu amesema, hivi sasa Serikali kupitia Wizara hiyo inatoa chanjo tisa (9) ikiwa ni kinga dhidi ya magomjwa 13 yakiwemo magonjwa ya kifua kikuu, Kupooza, Kifaduro, donda Koo, Pepopunda, homa ya ini, Kichomi, Uti wa mgongo, Mafua makali, kuhara, Surua, Rubella na Saratani ya mlango wa kizazi.
“Ni dhahiri kuwa haya ni mafanikio makubwa ikilinganishwa na mwaka 1975 tulipokuwa tukitoa chanjo dhidi ya magonjwa ya matano tu” amesema Waziri Ummy.
Aidha, amesema zoezi la Kampeni hiyo litagharimu takribani Tsh. Bilioni 11.9 sawa na dola za kimarekani Milioni 4.59 huku lengo kuu likiwa ni kushiriki katika mkakati wa kimatifa katika kutokomeza ugonjwa wa surua na Rubella ili kuchangia katika kupunguza vifo vya watoto hapa nchini.
Waziri wa afya Ummy Mwalimu akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Regina Chonjo.
Waziri Ummy amesema tayari Tanzania imefanikiwa kufikia lengo la Milenia la kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka vifo 104 kati ya vizazi hai1000 kwa mwaka 2004/2005 hadi vifo 54 kati ya vizazi hai 1000 mwaka 2013.
Naye mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk. Ketsela Mengistu amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutokomeza magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.
Dkt. Ketsela amewataka watanzania kushiriki kikamilifu katika Kampeni hizo ili kusaidia kupunguza vifo vya watoto vinavyotokana na magonjwa hayo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Loata Ole Sanare amesema, Jumla ya watoto 328, 462 wanatarajiwa kupata chanjo ya Surua na Rubella huku watoto 136,764 watapatiwa chanjo ya Polio Mkoani humo.
Amesema, Kampeni hizo hufanyika kila baada ya miaka mitatu ambapo mara ya mwisho ilifanyika mwaka 2014 wakati chanjo ya Rubella ilipoanza kutolewa kwa mara ya kwanza ambapo ilianza kwa watoto wa chini ya miaka 15.
Kampeni hii inatarajiwa kufanyika kitaifa kwa siku tano (5) kuanzia Oktoba 17 hadi Oktoba 21 itakapohitimishwa huku kauli mbiu ya Kampeni hiyo ikiwa ni “Chanjo ni Kinga , kwa pamoja tuwakinge”
mwisho
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.