Na Andrew Chimesela, Morogoro.
Wito umetolewa kwa Kampuni ya Watumishi Housing (WHC) pamoja na makampuni mengine yanayowekeza kwenye nyumba, kuwekeza Mkoani Morogoro kwa kuwa mji huo kwa sasa uko kimkakati na unapatikana katikati ya Miji miwili muhimu ya Dar es Salaam na Dodoma.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo wakati wa maonesho ya NMB Nyumba Day yaliyofanyika karibu na viwanja vya fire Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Maonesho hayo ambayo yaliratibiwa na Benki ya NMB yalishirikisha makampuni mbalimbali yanayojishughulisha na ujenzi wa nyumba na uuzaji wa vifaa vya ujenzi kwa kushirikiana na Benki ya NMB ili kufanikisha maadhimisho hayo.
Akiongea kwenye banda la Watumishi Housing wakati wa kutembelea mabanda ya maonesho, Mhandisi Kalobelo aliwataka Watumishi Housing kuanza kufikiria kuanzisha mradi mkubwa wa kuwekeza nyumba Morogoro kwa kuwa kwa sasa kuna kila dalili ya watu wengi kuhamia na kuishi Mkoani humo.
Amesema Kwa uamuzi wa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali katika Jiji la Dodoma na ujio wa Reli ya Mwendo kasi–SGR, ameuongezea kasi mji wa Morogoro haraka kwa kuwa watu wanatamani kuishi Morogoro na kufanya kazi Dodoma au Dar es Salaam hivyo Watumishi Housing wajipange kuanzisha mradi mkubwa wa kujenga nyumba za kutosheleza watu hao.
“wengi ukiangalia sasa hivi tunaopata wageni hata Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, wengi wanapenda kuishi Morogoro, hilo tayari ninyi wawekezaji upande wa nyumba linawapa picha kabisa.. kubuni mradi mkubwa wa kuhakikisha kwamba kunakuwa na nyumba za kutosha ndani ya Mkoa wa Morogoro”. Alisema Mhandisi Kalobelo.
“na unajua tuna ujio wa SGR sasa, treni ya mwendokasi, inakuja hapa, hii yenyewe inaleta soko kwa nyumba kwa sababu mtu atakuwa ana uwezo wa kuishi Morogoro akafanya kazi Dar es Salaam, akaishi Morogoro akafanya kazi Dodoma, sasa hiyo iwe chachu kwenu badala ya kusubiri watu kuja kujiandikisha hapa” alisisitiza Kalobelo.
Katika hatua nyingine ameyataka makampuni mbalimbali yanayojishughulisha na uuzaji wa nyumba au vifaa vya ujenzi wa nyumba kushusha bei zao ili wananchi wengi waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na Benki ya NMB ambayo inakusudia kusaidia watanzania wenye kipato cha chini kumiliki nyumba Bora.
Maoni hayo yalipokelewa na mwakilishi wa Watumishi Housing ambaye alieleza kuwa Watumishi Housing awali walikuwa wanauza nyumba kwa watumishi wa Umma pekee, lakini kulingana na mahitaji kuongezeka kwa sasa wanauza nyumba hizo pia kwa wafanyakazi wa Sekta binafsi pamoja na wananchama wote wa mifuko ya Jamii yaani PSSF, NSSF na Bima ya Afya.
Kwa upande wake Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Mashariki Dismas Prosper alitaja aina Nne za mikopo inayotolewa na Benki kuwa ni mkopo wa kununua nyumba mpya, mkopo wa kujenga nyumba mpya, Mkopo wa kumalizia ujenzi wa nyumba na Mkopo kwa mtu mwenye nyumba lakini anahitaji fedha kwa ajili ya shughuli nyingine.
Nao washiriki wa Maonesho hayo ambao wanashirikiana kwa karibu na Benki ya NMB katika biashara zao walieleza madhumui ya kushiriki maonesho pamoja na kazi wanazozifanya akiwemo Salvatori Vicent Tarimo wa Kampuni ya RAHISI BRICKS PROJECT anayejishughulisha na utengenezaji wa tofali za kuchoma, alisema wanapatikana Tuliani katika Wilaya ya Mvomero ambapo kila tofali wanaliuza kwa shilingi 150 huku gharama za usafirishaji zikiwa juu yao.
Pia amesema wanatarajia kuuza matofali hayo katika maeneo ya jirani hususan Morogoro Mjini na maeneo mengine ya karibu huku wakiwa na matarajio makubwa ya kuongezeka kwa wateja kutokana na huduma bora ambayo wanaitoa.
MWISHO.
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.