Watumishi RS Morogoro mwagiwa sifa, washauriwa kushiriki kupiga kura.
Na, Andrew Chimesela, Morogoro
Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wamepongezwa na Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo kwa kufanya kazi kwa bidii hivyo kuwaondolea wananchi kero mbalimba walizozifikisha ofisini hapo.
Mhandisi Kalobelo ametoa pongezi hizo kwa watumishi hao Oktoba 23 mwaka huu katika kikao kilichoshirikisha Wakuu wa Idara na Vitengo katika Ofisi hiyo ili kuwakumbusha kutekeleza majukumu yao lakini pia kutathmini utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Akizungumzia suala la kufanya kazi kwa bidii, Mhandisi Kalobelo amesema Watumishi katika Ofisi hiyo wametembea na kauli mbiu ya Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya “HAPA KAZI TU” kwa kuwa wamejituma kufanya kazi kwa bidii hususan katika kuwaondolea adha wananchi wa Mkoa huo kupitia ushauri wa kitaalamu walioutoa.
“kingine ambacho kimenipa faraja kufanya kazi na ninyi, ni pale tunapowataka mtoe maelezo Fulani au utaalamu Fulani kwa kweli mnajitahidi kutoa ushauri wa kitaalamu” alisisitiza Mhandisi Kalobelo.
Katika hatua nyingine Katibu Tawala huyo wa Mkoa ambaye ndiye mwajiri wa watumishi hao ametoa wito kwa watumishi wote kushiriki kikamilifu kwenye zoezi muhimu la Uchaguzi Mkuu katika kuchagua viongozi kwa nafasi ya Urais, Ubunge na Madiwani, ambalo linatarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.
Akimwakilisha Katibu Tawala Msaidizi Utumishi na Utawala, Victor Ndiva ambaye ni Afisa Tawala amesema ingawa kikao hicho ni cha kawaida ambacho hufanyika ili kuwakumbusha watumishi kutekeleza wajibu wao, kikao kimejikita katika kutathmini namna nzuri ya utoaji huduma kwa wananchi ili kuenenda na lengo la Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli ya kumsaidia mwananchi hususan wa hali ya chini.
Kwa upande wake Annamary Mwasendwa mmoja wa watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa amewakumbusha wananchi kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupata huduma wanazohitaji bila kutumia ushawishi wowote katika kupata huduma hiyo ikiwa ni pamoja na kutomshawishi mtoa huduma hiyo kumpa zawadi, kwani kufanya hivyo ni sawa na kutoa rushwa.
Naye ni Enock Juriely ambaye ni Afisa Elimu anayeshughulikia Elimu kwa TEHAMA, ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuratibu vema kikao hicho ambacho ndani yake wamejifunza mbinu mpya za utoaji huduma kwa wananchi hivyo kuendelea kutoa huduma hiyo kwa ubora zaidi.
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.