Watumishi RS Morogoro wakumbushwa kujiandaa kimaisha.
Na Andrew Chimesela – Morogoro
Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro wamekumbushwa na kuhimizwa kujiandaa kimaisha kwa kupanga mipango yao vizuri kuanzia sasa badala ya kutegemea kupanga mipango hiyo baada ya kustaafu.
Rai hiyo imetolewa Agosti 12 mwaka huu na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo alipozungumza nao muda mfupi baada ya Maafisa wa Benki ya NMB kufika na kutoa mada kuhusu huduma zinazotolewa na Benki hiyo na kuwahamasisha watumishi hao kwenda kuchukua mikopo iliyo na riba nafuu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo akiongea na Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa (Hawapo pichani)
Mhandisi Kalobelo amesema Mtumishi wa Serikali akiwa na uhakika wa maisha ya baadae ni dhahiri anaweza kufanya kazi vizuri katika utumishi na hata kuishi maisha marefu baada ya utumishi wake kuliko kama atakuwa hana uhakika wa maisha kutokana na kutojiandaa mapema kimaisha.
“tujitahidi kwa kadri tunavyoweza tuwe na mipango mizuri ya kuitumia mishahara yetu kwa kupata mikopo kwenye instituions (Taasisi) zilizopo” Amesema Mhandisi Kalobeli
Meneja wa Wateja Benki ya NMB Tawi la Wami Masanja Manyilizu akitoa mada kwa Watumishi wa RS Morogoro.
Aidha, amewatahadharisha watumishi hao kuchukua mikopo na kuanzisha miradi waliyoipanga wenyewe badala kuanzisha miradi kwa kufuata mikumbo ya watu na zaidi ametaka kupata ushauri wa kuanzisha miradi yao kutoka kwa Taasisi walizokopa fedha mikopo hiyo.
Katika hatua nyingine Kiongozi huyo ambaye ni mtendaji Mkuu wa Serikali ngazi ya Mkoa amesema nchi yetu ina Amani kwa muda mrefu ambayo inatokana na familia nyingi kuwa na amani, kwa msingi huo ametaka watumishi hao hususan ambao wako kwenye maisha ya ndoa kuishi maisha ya uaminifu ili Amani iweze kuimarika ndani ya familia na kudumisha msemo wa Tanzania ni kisiwa cha Amani.
Picha mbalimbali hapo juu ni Watumishi wa RS wakiwa katika Kikao hicho
Kwa upande wake Meneja wa Wateja kutoka Benki ya NMB tawi la Wami Mkoani hapa Bw. Masanja Manyilizu pamoja na kusisitiza kuwa Benki hiyo ina usalama wa uhakika katika kutunza pesa za wateja wao, amewataka watumishi hao kutokuwa na Imani yoyote katika masuala ya fedha hususan kutoa namba za siri za akaunti za benki kwani kufanya hivyo ni kuhatarisha usalama wa fedha zao.
Aidha, Manyilizu amewataka watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa kufika katika Benki yao na kupata mikopo ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikopo ya nyumba yenye riba ndogo badala ili kjiandaa mapema kimaisha kuliko kutegemea mishahara kwani mishahara yao ni daraja la wao kuwa na maisha bora.
Afisa Tawala Idara ya Utumishi na Utawala akiteta jambo na Afisa wa Benki ya NMB Tawi la Wami mara baada ya kikao hicho (picha zote na Andrew Chimesela)
MWISHO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.