Waziri Kakunda atoa wito
Waziri wa Viwanda na Biashara Joseph Kakunda amewataka watanzania kuondokana na dhana potofu iliyojengeka miongoni mwao ya kudharau bidhaa zinazotengenezwa katika viwanda vya hapa nchini badala yake ametoa wito kuzipende bidhaa hizo kwani zina sifa na ubora unaohitajika.
Waziri Kakunda ametoa wito huo Februari 16 mwaka huu wakati wa ziara yake ya siku moja Mkoani Morogoro alipotemmbelea Kiwanda cha kutengeneza Magunia na kiwanda cha kutengeneza nguo cha Twenty First Century ambavyo vyote viko Kihonda katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Baada ya kutembelea kiwanda hicho na kujionea mwenyewe nguo zinazotengenezwa kiwandani hapo huku zikiwa na ubora wa kimataifa, akatoa wito kwa Watanzania kutodharau bidhaa zinazotengenezwa hapa nchini badala yake kuzithamini na kuzipenda.
“watanzania hawapendi vitu ambavyo vimetengenezwa made in Tanzania wanadharau… Natoa wito kwa watanzania waanze kupenda vitu ambavyo vinavyotengenezwa Tanzania” alisema Waziri Kakunda.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe alimueleza Waziri Kakunda kuwa kiwanda cha Twenty First Century ambacho awali kilijulikana kama Morogoro Polyester ni moja ya viwanda 16 ambavyo vilijengwa na hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambacho pamoja na kiwanda cha Mazava kinachotengeneza nguo za michezo vinatoa ajira kwa watanzania zaidi ya 5,000.
Aidha, Waziri Kakunda alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro pamoja na viongozi wengeni wa Mkoa huo kwa kusimamia ufufuaji na ujenzi wa viwanda Mkoani humo na kuufanya Mkoa wa Morogoro kuanza kurejea kwenye hadhi yake ya zamani ya kuwa Mkoa wa Viwanda.
Naye meneja Uzalishaji wa Kiwanda hicho cha Kutengeneza Nguo Bw. Clementi Munisi alisema kiwanda chao kina uwezo wa kutenngeneza nguo zenye viwango vyote Duniani na wanaweza kushindana na nchi yoyote Duniani katika soko la kutengeneza nguo.
Kabla ya kutembelea kiwanda cha nguo, Waziri Kakunda alitembelea kiwanda kinachotengeneza magunia ambapo aliagiza Uongozi wa Kiwanda kutofunga kiwanda hicho kwa kuwa Serikali imekwisha pokea changamoto za kiwanda na inazifanyia kazi.
Akitoa taarifa ya kiwanda, Meneja wa Kiwanda hicho Ndekirwa Mnyari alimweleza Waziri kuwa kiwanda kina uwezo wa kuzalisha magunia milioni kumi kwa mwaka na kwa sasa kinatengeneza magunia yasiyozidi milioni mbili tu kwa mwaka, aidha kiwanda kwa sasa kina magunia laki tano ambayo yamekosa soko hali inayosababishwa na uingizwaji wa magunia kutoka nje ya nchi.
AFISA HABARI
OFISI YA MKUU WA MKOA
MOROGORO
Haki Miliki © 2020 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.