Huduma za Maji

Sensa ya mwaka 2012 inaonesha kuwa Mkoa wa Morogoro ulikuwa na wakazi wapatao 2,206,706. Hadi mwezi Dicemba, 2014 Wakazi wanaopata maji Vijijini ni asilimia 58.52. Kati ya vijiji 835 vya Mkoa wa Morogoro vijiji 345 vina kamati za maji, idadi ya vyombo vya watumia maji (COWSOs) vilivyoundwa hadi sasa imefikia 85.

Utekelezaji wa Miradi katika Vijiji 10 katika kila Halmashauri

Miradi mikubwa ya vijiji 10 inatekelezwa katika jumla ya vijiji 75, kati ya vijiji hivyo, vijiji 38 miradi imekamilika, vijiji 29 miradi ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na vijiji 8 vipo katika hatua ya manunuzi ya Wakandarasi. Aidha katika utekelezaji huo, zaidi ya vituo 504 vimejengwa ambapo vinatoa huduma kwa watu wapatao 59,608, Jumuiya za watumia maji  (COWSOs) 71 zimeundwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.

Hali ya huduma ya maji mijini

Idadi ya watu wanaopata huduma ya maji mijini inakadiriwa kufikia 203,734 sawa na asilimia 77 ya wakazi wote waishio Mijini. Miji hiyo ni pamoja na Manispaa ya Morogoro, Kilosa, Gairo, Turiani, Mvomero, Mikumi, Ifakara na Mahenge. Mtandao wa maji safi umeenea kwa asilimia 83. Na mtandao wa majitaka umesambaa kwa asilimia 3.36.

Usimamizi wa rasilimali za maji

Usimamizi wa Rasilimali za Maji katika Mkoa wa Morogoro unafanywa na Ofisi za Maji Bonde la Wami/Ruvu (Kilosa, Mvomero, Morogoro na Gairo) na Ofisi za Maji Bonde la Rufiji (Ulanga, na Kilombero).

Kupitia Programu ya Maendeleo ya Maji, Mpango wa Usimamizi wa Pamoja wa Rasilimali za Maji, Bonde la Wami Ruvu, umeandaliwa na kukamilika. Utekelezaji wake utaanza mwaka huu wa fedha 2014/15. Kwa upande wa Bonde la Rufiji, Maandalizi ya mpango huu yanaendelea.