Miundombinu

Miundombinu ya Madaraja

Hadi kufikia mwaka 2014, Mkoa una madaraja 1,054. Kati ya hayo, madaraja 850 yako kwenye barabara zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) na mengine 204 yako katika barabara za wilaya, ikilinganishwa na madaraja 816  yaliyokuwepo katika barabara zote za Mkoa kabla ya mwaka 2005. Katika kipindi hiki cha miaka 9, kuna ongezeko la madaraja 238, ambalo ni sawa na asilimia 29.16.

Ujenzi wa Daraja la mto Kilombero lenye urefu wa mita 384 pamoja na maingilio yake yenye urefu wa Kilometa 9.142 umeanza, ambapo kiasi cha shilingi 53,214,395,756.87 zitatumika. Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameweka jiwe la Msingi la daraja hilo mwezi Agosti, 2014. Mkandarasi wa mradi huo ni M/S China Railway 15 Bureau Group Corporation kutoka China. 

Uendelezaji wa Miji.

Shughuli hii inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Makazi. Mji Mkuu wa Mkoa Morogoro unao mpango madhubuti unaoongoza maendeleo na matumizi endelevu  ya Ardhi.Mji huu unayo hadhi na mamlaka ya Manispaa.

Miji Mikuu ya Wilaya zote pia inayo Mipango ya matumizi ya ardhi (“Urban Land Use Plans”).  Mipango hii imesaidia sana katika kuzuia ukuaji na uendelezaji holela wa maeneo ya Makazi. Pia eneo la Makao Makuu ya Wilaya Mpya ya Mvomero limeandaliwa michoro ambayo inatosheleza kuwa mpango wa awali wa uendelezaji Mji huo wa Dakawa Sokoine.

Katika kila Wilaya kuna Miji Midogo ambayo tayari imeshakua na inaendelezwa Kimji. Miji  hii pia ina michoro ya viwanja ambavyo vingine vimeshapimwa.  Vilevile, kuna Mamlaka za Miji 6  zilizoanzishwa  

Utayarishaji wa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi Vijijini.

Kutayarisha Mpango wa matumizi ya ardhi ya kijiji hulenga kutenga maeneo ya ardhi hiyo ya kijiji kwa shughuli mbalimbali kijijini hapo.  Shughuli hizo ni pamoja na makazi, malisho, Kilimo, shughuli za UMMA, n.k. Mpango huu huondoa uwezekano wa shughuli mbili tofauti kutekelezwa katika eneo moja. Na hivyo kuiweka migogoro ya ardhi katika hali ya kuweza kutatulika kwa njia bora zaidi.

 Mkoa wa morogoro una vijiji 614, kati ya hivyo vijiji 180 vimeandaliwa mipangi ya matumizi bora ya ardhi. katika kipindi cha mwaka 2013 na 214 jumla ya vijiji 180 vimeandaliwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ikilinganishwa na vijiji 118 vilivyoandaliwa mwaka 2010 sawa na ongezeko la vijiji 82 ( 65.5%). 

Migogoro ya Ardhi Vijiji:

Mkoa wa Morogoro umekuwa unakabiliwa na uwepo wa migogoro mingi ya ardhi na hivyo kuathiri shughuli za ushiriki wa wananchi katika shughuli mbalimabali za kiuchumi. migogoro mingi iliyopo katika Halmashauri ni ile ya mipaka ya vijiji na viwanja mjini, kumbukumbu zilizopo ni kuwa ipo jumla ya migogoro ya ardhi 90 katika mkoa kwa mgawanyiko ufuatao: Kilosa 7, Mvomero 14, Ulanga 10, halmashauri ya Morogoro 28, Kilombero 18 na Manispaa ya Morogoro 13. Uwepo wa migogoro hii unasababishwa na sababu zifuatazo:- 

· kutokuwepo kwa alama za mipaka ya vijiji.

· kutokutengwa kwa matumizi mbalimbali ya ardhi katika vijiji.

· migogoro inayosababishwa na mila na desturi.

· uvamizi katika maeneo ya Hifadhi pamoja na Ardhi ya kawaida.

· uwepo wa ukiukwaji wa sheria kwa viongozi wa vijiji.

· kutosimamiwa vizuri kwa mipango ya matumizi bora ya Ardhi katika vijiji.

 · migogoro katika vitalu vya uwindaji.