Mkoa wa Morogoro

Mkoa wa Morogoro ni Mkoa wa pili kwa ukubwa nchini ukitanguliwa na Mkoa wa Tabora. Mkoa una eneo la kilometa za mraba 73,039. Eneo hili ni sawa na asilimia 7.7 ya eneo lote la Tanzania Bara, kati ya eneo hili Km2 2,240 ni eneo la maji. Mkoa umepakana na Mikoa ya Pwani na Lindi kwa upande wa Mashariki, Manyara na Tanga upande wa Kaskazini na kwa upande wa Magharibi umepakana na Mikoa ya Dodoma na Iringa. Upande wa Kusini unapakana na Mkoa wa Ruvuma. 

Hali ya Hewa

Mkoa hupata mvua mara mbili kwa mwaka. Mvua za vuli hunyesha kuanzia mwezi Oktoba hadi katikati ya mwezi Januari, na mvua za masika hunyesha katikati ya mwezi Februari na kuishia mwezi Mei mwishoni. Kiwango cha mvua ni kati ya milimita 600 katika sehemu za tambarare na milimita 1,200 katika miinuko. Hata hivyo, zipo sehemu zilizo na ukame ambazo hupata mvua chini ya milimita 600 kwa mwaka. Sehemu hizo ni pamoja na Tarafa za Gairo katika wilaya ya Gairo, Mamboya katika Wilaya ya Kilosa na Tarafa ya Ngerengere katika Wilaya ya Morogoro.

Utawala

Mkoa wa Morogoro kiutawala umegawanyika katika Wilaya sita ambazo ni Wilaya za Morogoro, Mvomero, Kilosa, Kilombero, Ulanga na Gairo. 

Kufuatana  na Muundo wa Serikali za Mitaa Mkoa una Halmashauri sita za Wilaya  na Halmashauri ya Manispaa moja. Halmashauri za Wilaya ni pamoja na Kilosa, Gairo, Kilombero, Morogoro, Ulanga, Mvomero na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro. Mkoa unayo majimbo ya Uchaguzi 10, Kata 212, Vijiji 673, Mitaa 295, vitongoji 3,451  

Idadi ya watu

Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na  Makazi ya mwaka 2012  idadi ya kaya za Mkoa wa Morogoro ni 489,688 zenye watu 2,218,492 ambapo  kati yao wanawake ni 1, 125,190 na wanaume ni 1,093,302.  Wastani wa idadi ya watu katika Kaya ni 4.5.