Watendaji wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wamepongezwa kwa utendaji mzuri katika utekelezaji wa shughuli za Serikali kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 ambayo imetekelezwa kwa asilimia 96.
Pongezi hizo zimetolewa Septemba 07 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabir Makame kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu El-Maamry Mwamba wakati akifunga kikao kazi cha siku tatu cha tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya 2022/2023 na maandalizi ya bajeti ya 2023/2024 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa NSSF uliopo Manispaa ya Morogoro.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabir Makame akizungumza na washiriki wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema ushirikiano katika kutekeleza bajeti hiyo umewezesha kupata mafanikio katika utekelezaji wa shughuli za Serikali ambapo kwa asilimia 96 shughuli hizo zimefanikiwa hivyo amewashukuru na kuwapongeza kwa ushirikiano na utendaji kazi mzuri.
“...nitumie fursa hii kuwashukuru kwa ushirikiano na utendaji kazi mzuri katika utekelezaji mzuri wa bajeti ya 2022/2023 uliotuwezesha kupata mafanikio ambapo kwa asimilia 96 tumefanikiwa...” amesema Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabir Makame.
Aidha, amesema kuwa Serikali itayafanyia kazi maoni yaliyotolewa na washiriki wa kikao hicho kwa kuwa wao ndiyo watekelezaji wakubwa wa bajeti katika maeneo yao.
Sambamba na hilo Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabir Makame amesema Serikali imezipokea changamoto zilizoibuliwa na wajumbe wa kikao hicho hususan katika uandaaji wa bajeti na kuahidi kuzifanyia kazi ili kuboresha utekelezaji wa bajeti hiyo.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Sehem ya Mipango na Uratibu Bw. Anza-Ameni Ndosa amesema kikao hicho kimelenga kujadili changamoto mbalimbali za utekelezaji wa bajeti na namna ya kutatua changamoto hizo.
Katibu Tawala Msaidizi Sehem ya Mipango na Uratibu Bw. Anza-Ameni Ndosa akiwa kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali 2022/2023.
Naye, Bw. Edson Toto ambaye ni Mchumi kutoka Wizara ya Fedha amesema kikao hicho kimehusisha washiriki kutoka Mikoa 13 ambapo Maafisa Mipango wa Mikoa na Halmashauri, Maafisa Rasilimali watu na Wahasibu ni walengwa wa kikao.
Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wa kikao hicho Katibu Tawala Msaidizi Sehem ya Mipango na Uratibu wa Mkoa wa Njombe Bw. Edward Mwakipesile ameshukuru na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo waliyoyapata kwenye mafunzo ili kupata mafanikio chanya katika utekelezaji wa shughuli za Serikali katika maeneo yao.
Katibu Tawala Msaidizi Sehem ya Mipango na Uratibu kutoka Mkoa wa Njombe Bw. Edward Mwakipesile akitoa neno la shukran kwa mgeni rasmi pamoja na kwa waandaaji wa kikao kazi hicho.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.