Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kuongeza ubunifu katika kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje hivyo kuongeza Uchumi wa nchi kwa maslahi ya taifa.
Waziri Kijaji amesema hayo Novemba 24, 2025, alipotembelea makao makuu ya TAWA yaliyopo mkoani Morogoro ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Waziri mwenye dhamana ya Wizara hiyo.
Amesema, ni muhimu kutumia mbinu mbalimbali katika kutangaza vivutio vilivyopo ili viweze kunufaisha taifa, pamoja na kuibua vivutio vipya vilivyopo katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili viweze kujulikana na kuongeza watalii, hatua ambayo itaongeza mapato na kuimarisha uhifadhi wa maliasili.
“...tuongeze juhudi za utangazaji wa vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo yetu yote ya TAWA ili kuongeza idadi ya watalii wa ndani na nje...” amesema Dkt. Ashatu Kijaji
Aidha, Dkt. Ashatu ameitaka mamlaka hiyo kuendelea kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia utu na kusisitiza kuwa migongano baina ya TAWA na wananchi lazima ishughulikiwe kwa haraka ili wananchi waweze kufanya shughuli zao bila kuathiriwa na uharibifu unaoweza kusababishwa na wanyamapori.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mlage Yusuph Kabange, amewataka wananchi kuendelea kufuata sheria kwa kutoingia au kuvamia maeneo ya uhifadhi na kufanya shughuli za kibinadamu, jambo ambalo amesema lina sababisha uharibifu wa maeneo hayo.
Ameongeza kuwa, wataalamu wa mamlaka hiyo wana jukumu la kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, pamoja na kuhakikisha wananchi wanafuata maelekezo wanayopewa na Serikali kupitia wataalamu kuhusu mbinu za kujikinga na wanyamapori ili kuboresha uhifadhi na usalama wa jamii.
Naye Mwenyekiti wa Bodi, Meja Jenerali Khamisi Semfuko, amesema kuwa bodi imejipanga kuongeza ukusanyaji wa mapato ambapo mwaka 2027/2028 TAWA inatarajiwa kuwa na makusanyo ya zaidi ya shilingi bilioni 187. Aidha, amewataka watendaji kuendelea kufanya kazi kwa ubunifu ili kufikia malengo waliyojiwekea na kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za taifa.
Katika tukio hilo Waziri Kijaji amegawa vitendea kazi kwa watumishi wa TAWA ikiwa ni pamoja na magari, pikipiki, ndege nyuki (drowns) kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa utendaji kazi ndani ya Taasisi hiyo.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255719112299
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.