Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Adolph Ndunguru ametoa siku 45 kwa wadau wanaotekeleza mradi wa Uendelevu wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Sustanable, Rural Water Supply and Sanitation – SRWSS)kukamilisha miundombinu ya mradi huo ambayo haijakamilika.
Katibu Mkuu Adolph Ndunguru ametoa agizo hilo leo Julai 17,2024 wakati akifunga kikao kazi hicho cha siku mbili kilichofanyika Mkoani Morogoro kikiwahusisha waganga Wakuu wa Mikoa na Maafisa Afya wa Mikoa yote Tanzania Bara lengo likiwa ni kujitathmini juu ya utekelezaji wa Mradi huo.
Amesema Mpaka sasa mradi wa SRWSS umefikia vituo vya kutolea huduma za Afya 2,727 na shule za Msingi 1,842, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya vituo vya kutolea huduma za Afya 838 na shule 566 vimepokea fedha za utekelezaji huku zaidi ya asilimia 60 ya vituo hivyo vikiwa vimekamilika.
Kwa sababu hiyo, Katibu Mkuu Ndunguru amesema kwa sasa hakuna kisingizio chochote cha kutokamilisha ujenzi wa miundombinu kwa asilimia 40 zilizobaki na kuwataka wadau wa mradi huo kutekeleza ujenzi wa miundombinu hiyo kabla au ifikapo Agosti 30 mwaka huu.
“Nichukue fursa hii kuwataka wadau wote wanaohusika na utekelezaji wa mradi huu, kusimamia asilimia 40 ya miradi ambayo haijakamilika ili ikamilike kabla ya, au ifikapo tarehe 30 Agosti, 2024” amesema Katibu Mkuu.
Pamoja na agizo hilo Katibu Mkuu wa TAMISEMI amesema kukamilika kwa miradi yote hiyo kutaimarisha Afya za watanzania wa maeneo husika na kuwafanya kushiriki kikamilifu katika kujenga Uchumi wao na Uchumi wa Taifa kwa jumla.
Katika hatua nyingine Kiongozi huyo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuijali Sekta ya Afya ikiwemo kuboresha bajeti yake, kutoa kwa wakati vitendea kazi na fedha za uendeshaji.
Sambamba na pongezi kwa Serikali, ameupongeza Mkoa wa Kagera kwa kufikisha asilimia 85 ya ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za Afya na kuitaka Mikoa mingine kuiga mafano huo mzuri wa ufanisi kwa kutekeleza malengo yanayotolewa na Serikali.
Akizungumzia ugonjwa wa Kipindupindu uliojitokeza siku za hivi karibuni kwa baadhi ya mikoa hapa nchini ikiwemo mikoa ya Manyara, Singida, Dodoma Lindi, Kigoma na Mara, Katibu Mkuu Adolph Ndunguru amesema uimarishaji wa usalama wa maji, ujenzi na matumizi ya vyoo bora ni moja ya silaha ya kutokomeza magonjwa ya mlipuko ukiwemo ugonjwa huo.
Hivyo, ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuzingatia kanuni Bora za Afya ikiwemo unawaji mikono kwa maji tiriri na sabuni kwa lengo la kuudhibiti ugonjwa huo na watendaji kusimamia eneo hilo.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Anyantike Mwakitalima amesema mradi huo umefanyika kwa mafanikio hususan ukilinganisha malengo na kazi iliyofanyika huku akibainisha kigezo kimojawapo kuwa kaya zenye watu zaidi ya 10,000 zimefikiwa na kutoa elimu ya kuwa na vyoo bora na kuvitumia huku lengo likiwa ni kuzifikia kaya zenye watu 9,000.
Naye Mratibu wa Mradi wa Uendelevu wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (SRWSS) kutoka TAMISEMI Bw. Seleman Yondu amesema mradi huo ulioanza mwaka 2019/2020, kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 umepokea jumla ya Tsh. 83.1Bil kwa ajili ya utekelezaji wake huku Sekta ya Afya ikitumia shilingi Bil. 54.39 na ujenzi wa miundombinu ya Elimu ikitumia shilingi Bil. 28.73
Amesema, Mradi unatekelezwa katika mikoa yote 25 ya Tanzania bara na Halmashauri 137, huku akiweka bayana kuwa Manispaa, miji na majiji sio sehemu ya mradi huu.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Best Magoma ambaye katika kikao hicho alimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa, Pamoja na kuishukuru serikali kwa kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za Afya ameiomba Serikali usafiri wa pikipiki kwa ajili ya watendaji wa kutoa huduma za Afya ngazi ya chini ili kuwawezesha watendaji hao kufika kila kaya na kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Naye Afisa Afya Mkoa wa Morogoro Bi. Prisca Laurent kwa niaba ya washiriki wengine amesema kufanya vizuri katika mradi huo utapunguza magonjwa ya mlipuko lakini pia kuziwezesha Halmashauri kupewa fedha zaidi.
Aidha, amebainisha kuwa uhamasishaji wa kujenga na kutumia vyoo bora kwa wananchi wa Mkoa huo umeongezeka kutoka asilimia 72 hadi 73 na kwamba Mkoa huo kuanzia mwaka 2023 tayari umepokea zaidi ya Tsh. 3 Bil. Kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.