Hapa Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Peter Pinda anasalimiana na baadhi ya viongozi na wadau wa sekta za kilimo, ufugaji na Uvuvi mara baada ya kuwasili katika Viwanja vya Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ya ufunguzi wa maonesho hayo.
Serikali imeendelea kuweka mpango mkakati kwenye sekta ya kilimo ambacho kitachangia 10% ya Pato la Taifa ifikapo 2030 hivyo kukuza uchumi wa Taifa.
Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Peter Pinda akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika Viwanja vya Julius Kambarage Nyerere kwa ajili ufunguzi wa maonesho ya Nane nane kanda ya Mashariki 2023.
Kauli hiyo imetolewa na Mhe. Mizengo Pinda Waziri Mkuu mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Agosti 1, 2023 wakati akifungua maonesho ya wakulima na wafugaji maarufu kama Nanenane Kanda ya Mashariki yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere vilivyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkoani Morogoro.
Mhe. Mizengo Pinda amesema mipango hiyo itawawezesha wakulima kulima kilimo chenye tija ambacho kitasaidia kuchangia kiasi kikubwa katika pato la Taifa, hata hivyo amethibitisha uwepo wa hekta milioni 44 za ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo ambapo 15% ya ardhi hiyo ndiyo pekee inatumika kwenye kilimo.
“…Kwa hiyo ndugu huu mpango ambao tunakuja nao tunataka tuone unaleta matunda ndani ya muda mfupi kadri itakavyowezekana lakini lengo kubwa mpaka ifikapo 2030 tuwe tumesukuma kilimo kiweze kuchangia angalau 10%...” amesema Mhe. Mizengo Pinda
Mhe. Mizengo Peter Pinda akipokea zawadi kutoka kwa wataalam wa Taasisi ya utafiti wa kilimo TARI baada ya kutembelea banda hilo.
Aidha, Mhe. Pinda amezitaka halmashauri kote nchini kuchukua kundi kubwa la vijana sambamba na wanawake kushirikiana nao ili kukuza zaidi uchumi kwani vijana ndio nguvu kazi ya Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba akiwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge wakati wa mapokezi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mizengo Peter Pinda ambaye ni mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa maonesho hayo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Pinda amesikitishwa na udumavu wa watoto chini ya miaka 5 ambapo mama anakuwa amekosa lishe bora kwa maandalizi ya mtoto kuwa na afya bora, hata hivyo ameweka bayana kuwa Mkoa wa Morogoro una tatizo la udumavu kwa 30.6% ambapo mwanzo ilikuwa 35% ikiongozwa na Iringa yenye 56.9%, wakati Mkoa huo ni Mkoa wa uzalishaji wa chakula cha kutosha katika maeneo mengi.
Hapa Mhe. Mizengo Peter Pinda akiwa pamoja na viongozi mbalimbali na wadau wa kilimo, ufugaji na Uvuvi wakimsikiliza mtaalam kutoka Bodi ya sukari akielezea teknolojia ya upigaji dawa kwa kutumia ndege ndogo isiyo na rubani.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mizengo Pinda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongeza bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kufikia bilioni 970 huku akitaka fedha nyingi zielekezwe katika Sekta ya kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji wa mbegu bora, mbolea na viwatilifu wakati 2022/2023 bajeti ilikuwa bilioni 751.1 na 2021/2022 ilikuwa bilioni 294.2, hivyo kadri miaka inavyozidi kwenda na kasi inaongezeka Zaidi.
Kwa upande wake, Mhe. Adam Kighoma Malima, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amesema miundombinu kama barabara katika Mkoa huo ni jambo la lazima kwani Mkoa huo umejipanga kuzalisha mazao ya kibiashara ikiwemo mpunga, wakati mkoa huo unauwezo wa kuzalisha tani milioni 2 za zao hilo, hivyo miundombinu ni suala muhimu kwa uchumi wa Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akimuelezea jambo Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda katika banda la TARI.
Naye, Mhe. Abubakar Kunenge Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya Maonesho ya Nanenane kanda ya mashariki amesema kanda hiyo imejipanga kufanya vizuri katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji kwani kanda hiyo ni kinara wa viwanda vikiwemo viwanda vya sukari na kuwataka wananchi kushirikiana vema na wataalamu ili kulima kilimo chenye tija zaidi.
Mhe. Mizengo Peter Pinda akimsikiliza mtaalam wa TARI akielezea bidhaa zinazopatikana katika banda hilo.
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Peter Pinda akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na wafanyakazi wa TARI
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.