Zaidi ya wananchi 2.1Mil. Mkoani Morogoro waliojiandikisha kupiga kura, kesho Oktoba 29, 2025 wanatarajia kupiga kura ya kuchagua Madiwani, Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima akibainisha kuwa hali ya Ulizi na Usalama ndani ya Mkoa huo iko shwari.
Mhe. Malima amebainisha hayo leo Oktoba 28, 2025 wakati wa Mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuzungumzia maandalizi ya uchaguzi wa kesho wenye kaulimbiu ya "kura yako haki yako, jitokeze kupiga kura".
Amesema, hali ya ulinzi na usalama ndani ya Mkoa umeimarishwa katika kukabiliana na wanaotaka kuleta vurugu huku akisisitiza wananchi wote 2, 114,052 waliojiandikisha kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kutimiza haki yao ya msingi na ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kwa maslahi mapana ya Taifa.
".. Nataka niwahakikishie wanamorogoro wenzangu kwamba nendeni mkapige kura tuko vizuri....kwenye upande wa ulinzi na usalama.." amesema Mhe. Adam Malima
Aidha amesema, Mkoa huo ulifanya vizuri katika zoezi la uandikishaji wa wapiga kura, sanjali na zoezi la kuboresha taarifa za Mpiga Kura na kubainisha kuwa Mkoa huo una jumla ya vituo vya kupigia kura 5,860 ambapo Vituo hivyo vimeandaliwa vizuri na viko tayari kwa ajili ya siku ya uchaguzi wa Octoba 29, 2025.
Katika hatua nyingine Malima amebainisha kuwa vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia Saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 Jioni na kutoa wito kwa wananchi wenye sifa ya kupiga kura kuwahi kwenda kupiga kura na kuwaonyo wenye nia ya kuleta vurugu wakati wa zoezi hilo kuwa watachukulia hatua kali za kisheria.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa huo Kamishna mstaafu wa jeshi la Polisi Alhaji Dkt. Mussa Ali Mussa amezungumzia jografia ya Mkoa huo na kwamba mazingira hayo yanaweza kusababisha ucheleweshwaji wa taarifa za matokeo ya upigaji kura kwa baadhi ya maeneo, muhim ni wananchi na waandishi wa habari kuwa na subira.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.