HPSS yafunga Ofisi za Kanda, huku mradio huo ukiwa bado unahitajika
Mradi wa Tuimarishe Afya (HPSS) ambaao umekuwa ni mdau mkubwa katika Sekta ya Afya hapa nchini umefunga Ofisi zake za Kanda na kubakiza Ofisi za HPSS Taifa pekee huku ikielezwa kuwa mradi huo bado unahitajika hususan wakati huu ambapo Serikali inaelekea kuanzisha Bima ya Afya kwa wote kipindi kifupi kijacho.
Mgeni rasmi ambaye pia ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozaria Rwegasira akiwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Ukio Kusirye
Kauli hiyo imetolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dkt. Gunini Kamba wakati wa kikao cha kufunga Ofisi za Mradi wa HPSS Kanda ya Mashariki kilichofanyika Oktoba 22 mwaka huu katika hoteli ya Glonence iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Technical Officer wa Mradi wa HPSS Kanda ya Mashariki Alicia Mwashilindi
Dkt. Kamba amesema pamoja na kuwapongeza HPSS kwa kazi nzuri walizofanya kwa kipindi kifupi ikiwemo kuongeza usajiri kwa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii uliyoboreshwa - ICHF, masuala ya usambazaji na menejimenti ya dawa – JAZIA, na kazi nyingine nyingi, bado amesema Mradi huo bado ulikuwa unahitajika katika kanda hiyo ya Mashariki husuan katika kipindi hiki ambacho Serikali inataka kuanzisha Bima ya Afya kwa kila mwananchi.
“kuna mambo ambayo tulikuwa tunaendelea kuyajenga, ukizingatia Serikali inelekea kuanzisha bima ya Afya kwa wote, kila mwananchi atatakiwa apate Bima ya Afya, sasa nao ndipo wanaondoka, tulitaraji huu mswaada ambao utapitishwa mwezi ujao Novemba labda tungeweza kukubaliana nao kusaidia kwenye suala la Bima ya Afya kwa kila Mwananchi” alisema Dkt. Kamba.
Baadhi ya Washiriki wa kikao kilichofanyika kwa ajili ya kufunga Ofisi za Kanda za Mradi wa HPSS
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Rozaria Rwegasira ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amewataka Wajumbe wa kikao hicho kuendeleza yote mazuri yaliyoazishwa na Mradi wa HPSS na kwamba anaamini hilo linawezekana kwa sababu viongozi wa mradi huo walifanya kazi kwa kushirikisha wajumbe wa RHMT wa Mikoa yote husika ya Dar, es Salaam, Pwani na Morogoro.
Aidha amesema, ipo kasumba hapa nchini ukiwemo Mkoa wa Morogoro kutoendeleza miradi inayoaazishwa, amesema baada ya mradi kuanzishwa na mradi unapofika kikomo chake cha ufadhiri na mradi nao hufa na kwamba hangependa hilo litokee ndani ya mikoa hiyo ya Kanda ya Mashariki.
Badala yake amewataka wajumbe wa kikao hicho kuendele kufanya mawasiliano na Viongozi wa HPSS wa Ofisi za Taifa ili kama kuna jambo halikukamilika au kueleweka yafanyike mawasiliano na Ofisi hizo zilizopo Jijini Dodoma ili kupata ufafanuzi wa jambo hilo na kupatiwa ufumbuzi, lengo ni kuendeleza kazi za utoaji wa huduma ya Afya kwa wananchi kwa ufanisi zaidi.
“Kuna kawaida miradi mingi inayoanzishwa nchini kwetu, hata hapa Morogoro inakuwa haina mwendelezo, mradi unaanza ukifika mwisho inakuwa ndio mwisho wa maradi. Lakini mimi naamini kwenye mradi huu kwa kuwa kulikuwa na ushirikishwaji na timu za RHMT na wadau wengine mradi huu utakuwa ni endelevu” alisema Dkt. Rozalia.
Mratibu wa Mfuko wa Afya ya Jamii iliyoboreshwa - ICHF Mkoa wa Morogoro Alicia Mtesigwa, amekiri kuwa HPSS kama Mdau wa Afya, wamekuwa na mchango mkubwa katika Afua ya ICHF hususan katika uandikishaji, uhamasishaji na utoaji wa huduma za Bima hiyo kwa ngazi zote na kwa Halmashauri zote tisa za Mkoa wa Morogoro.
Aidha, Bi. Alicia amebainisha mikakati waliyoiweka baada ya kutambua kuwa mradi unakwenda kufika kikomo, lengo ni kuendeleza yote mazuri yaliyofanywa na HPSS bila kutetereka kwa kutenga bajeti kwa kila Halmashauri kwa ajili ya shughuli hizo zilizokuwa zinafanywa na Mradi wa HPSS.
Mratibu wa Mfuko wa Afya ya Jamii iliyoboreshwa - ICHF Mkoa wa Morogoro Alicia Mtesigwa
Akitoa taarifa ya kufunga Mradi wa HPSS kanda ya Mashariki na kubaka na Ofisi ya HPSS Taifa pekee ambayo itakuwa Jiji la Dodoma, Afisa wa HPSS wa kanda hiyo Bi. Alice Mwashilindi amesema Mradi wa HPSS ulikuwa unasaidia katika maeneo manne yaani uhamasishaji wa mfuko wa Bima ya Afya ulioboreshwa – ICHF, Uhamasishaji wa Afya Kinga, na kushughulikia mfumo wa usambaza madawa na menejimenti yake unaofahamika kama JAZIA katika maeneo ya kutolea huduma za Afya kama Hospitali na Vituo vya Afya.
Hata hivyo Bi. Alice amesema Mradi wa HPSS unapoelekea kufungwa kiutendaji katika Kanda hiyo yenye mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro anaamini kazi zilizoanzishwa na HPSS zitakwenda kuimarishwa na kuendelezwa kwa kuwa walifanya kazi kwa kuwashirikisha timu za kila Halmashauri na kwamba wataweza kwa sababu timu hizo kwanza zinamuundo mzuri
“tumeweza kuwajengea uwezo mkubwa kabisa kwa hiyo mpaka sasa tunaondoka kwenye ofisi zetu za kanda tukiwa na uhakika kabisa kwamba timu zetu za mikoa zina uwezo mkubwa wa kuzifanya zile shughuli walizokuwa wanazifanya kwa sababu tayari tumekwisha zijengea uwezo” alisema Bi. Alice.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.