Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabir Makame akizungumza na wadau wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoani Morogoro wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Mashirika hayo.
Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoani Morogoro yametakiwa kupanua wigo wa utoaji huduma kwenye jamii katika maeneo ambayo hayajafikiwa ili kutoa fursa ya sawa kwa huduma zinazotolewa.
Hayo yamesemwa Septemba 07 mwaka huu na Mkuu wa Wilaya ya Gairo Bw. Jabir Makame kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima wakati akifungua mkutano wa mwaka wa mashirika hayo yaliyopo Mkoani Morogoro uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Bw. Makame amesema baadhi ya mashirika hayo hutekeleza shughuli zake kwa kuchagua maeneo hususan maeneo ya mijini hivyo kupunguza fursa kwa maeneo mengine kupata huduma zinazotolewa na mashirika hayo, hivyo ameyataka mashirika hayo kuyafikia maeneo ambayo yanauhitaji hususan maeneo yaliyo pembezoni mwa mji.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabir Makame akibadilishana mawazo na mtaalam wa elimu kwa mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati wa mkutano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
“...naomba nitoe msisitizo kwamba katika kutekeleza majukumu yenu ni vyema pia kuangalia maeneo ambayo yanauhitaji vile vile ikiwemo katika Wilaya zingine za pembezoni...utakuta mashirika mengi yapo mjini...” amesema Jabiri Makame.
Aidha, amesema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inatambua mchango wa Mashirika hayo katika kuleta maendeleo kwenye sekta mbalimbali za Afya, elimu, maji, mazingira, kilimo, upingaji wa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na uimarishaji wa uchumi wa kaya.
Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa Wilaya ameyataka mashirika hayo kutojikita katika miradi ambayo ni kinyume na mila, tamaduni na maadili ya Watanzania na kwamba Serikali haitashindwa kuyachukulia hatua mashirika yatakayo jihusisha na ukiukaji wa tamaduni za watanzania.
Katibu Tawala Msaidizi Sehem ya Rasilimali watu na Utawala Bw. Herman Tesha akizungumza wakati wa mkutano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoani Morogoro.
Katibu Tawala Msaidizi Sehem ya Mipango na Uratibu Bw. Anza-Ameni Ndosa akifafanua kuhusu umuhimu wa mkutano hyo.
Kwa upande wao wadau wa Mashirika hayo Mkoani humo akiwemo Mjumbe wa Uratibu kutoka Taasisi ya Acts of Life Dkt. Francis Nyakamwe amebainisha changamoto zinazoyakabili mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoani humo zikiwemo ukosefu wa rasilimali fedha, sheria kandamizi zinazowabana katika utendaji kazi zao, wingi wa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo hawana uelewa nazo.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabir Makame akiwa kwenye picha za pamoja na makundi mbalimbali ya wadau wa Mashirika yasiyo Kiserikali baada ya ufunguzi wa mkutano hyo.
Aidha, wadau hao wamependekeza kuwepo kwa miongozo ya moja kwa moja ya usajili hii ni kutokana na changamoto ya mashirika hayo kutakiwa kusajiliwa kwa mara ya pili hususan kwenye maeneo wanayokwenda kutekeleza shughuli zao.
Kikao hicho kimelenga kujadili kwa pamoja namna ya kutatua changamoto zinazoyakabili mashirika hayo pamoja na Serikali kutoa maelekezo kwa mujibu wa sheria, kanuni na sera zinazotolewa mara kwa mara.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.