Baraza la Michezo ya Majeshi hapa nchini (BAMMATA) linatarajia kuanza kutimua vumbi Mkoani Morogoro kuanzia Septemba 6 hadi 15 mwaka huu ambapo mashindano ya michezo mbalimbali itafanyika na zaidi ya wanamichezo 1300 kutoka Kanda 8 za michezo hiyo hapa nchini watashiriki mashindano hayo.
Hayo yamebainishwa Agosti 17, mwaka huu na Mwenyekiti wa BAMMATA Brigedia Jenerali Said Hamis Said katika kikao na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi yake kikiwa na lengo la kujitambulisha na kutoa adhima ya kusudio la kuanzisha mashindano hayo Mkoani humo.
Akifafanua zaidi Brigedia Jenerali Said Hamis amesema mashindano hayo yatajumiisha kanda 8 ambazo ni Ngome, Ngome visiwani, polisi, magereza, ujamiaji, zimamoto, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Vikosi maalum vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kushiriki michezo mbalimbali Mkoani humo.
"... sisi kama Baraza la michezo la majeshi tumeona tuje Morogoro tuwe sehemu ya kuimarisha Ulinzi na Usalama kwa kuwakutanisha wanausalama wote kupitia michezo..." Amesema Brigedia Jenerali huyo
Kwa upande wake, Mhe. Adam Kighoma Malima ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amesema michezo huunganisha wananchi wote kuwa sehemu moja bila kujali chama, kabila hata tofauti zao hivyo amevipongeza vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kuanzisha mashindano hayo Mkoani humo.
Aidha, amesema mashindano hayo yana manufaa makubwa katika kuimarisha umoja wa kitaifa na kimataifa katika kuleta ushirikiano baina ya majeshi na wananchi sambamba na kuimarisha Ulinzi na Usalama na ustawi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania..
Hata hivyo Mhe. Adam Malima ameyataka mashindano hayo kuwa daraja la kubaini vipaji vilivyo ndani ya majeshi hayo na kuendelezwa ili kupata wanamichezo watakaoiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa kwa sababu hiyo amewataka wananchi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki michezo hiyo ili kuwapa nguvu majeshi yao na kujifunza michezo itakayochezwa.
Mashindano hayo yanayoratibiwa na BAMMATA hufanyika kila mwaka ambapo mwaka 2023 yalifanyika Mkoa wa Mtwara na mwaka 2024 kufanyika Mkoani Morogoro ambapo michezo inayotarajiwa kuwepo ni pamoja na mpira wa Miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, riadha na shabaha
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.