Mkoa wa Morogoro umefikisha asilimia zaidi ya 95 ya lengo waliojiwekea la kutokomeza maambukizi mapya ya VVU kutokana na Mkoa huo kuweka juhudi katika utoaji wa elimu ya kinga dhidi ya VVU kwa wananchi wake.
Hayo yamebainishwa Novemba 24, 2023 na Mhe. Adam Kighoma Malima Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakati akifungua wiki ya Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambayo kitaifa yanafanyika Mkoani humo.
Mhe. Kighoma Malima amebainisha kuwa Mkoa huo uliweka malengo yake katika kuwafikia wananchi na kutoa Elimu dhidi ya kutokomeza VVU na UKIMWI kwa makundi mbalimbali ya jamii hususan Vijana.
Jitihada nyingine zilizotumika katika kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa huo ni pamoja na kutoa huduma ya ushauri na saha na upimaji wa hiari, matunzo na matibabu kwa watu waishio na VVU(WAVIU), hivyo juhudi hizo zimefanya Mkoa huo kuvuka lengo la 95 tatu.
Aidha, Mhe. Malima amesema Mkoa huo umevuka malengo ya tisini na tano tatu (95, 95, 95) hadi kufikia mwezi Septemba 2023 amabapo wananchi wanaotambua hali zao za Maambukizi ya VVU baada ya kupimwa ni asilimia 98.8, Wanaotumia dawa Kati ya watu waliogundulika kuwa na VVU ni asilimia 95 na kati ya watu wanaoishi na VVU ambao wanatumia dawa za kufubaza VVU – ARV nao wamefikia asilimia 95.8.
“...tisini na tano ya kwanza wananchi wanaotambua hali zao za Maambukizi ya VVU baada ya kupimwa ni asilimia 98.8, tisini na tano ya Pili Wanaotumia dawa Kati ya watu waliogundulika kuwa na VVU ni asilimia 95 na tisini tano ya tatu inaonyesha kuwa kati ya watu wanaoishi na VVU ambao wanatumia dawa za ARV wamefubaza VVU ni asilimia 95.8…” amesema Mkuu wa Mkoa.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewashukuru wananchi wa Mkoa huo kwa kuwa na mwitikio chanya wa upimaji wa hiari ambapo kumekuwa na ongezeko la watu wanaopima VVU kila mwaka kutoka 226,213 kwa mwaka 2021, mpaka 292,731 kwa mwaka 2022 .
Hata hivyo amesema Mkoa umeendelea kutoa huduma za upimaji wa VVU ambapo kwa mwaka huu kuanzia Januari hadi Septemba jumla ya watu 100162 walipimwa, kati yao wanawake 61665 na wanaume 38497 na waliogundulika na maambukizi ya VVU walikuwa 1,884 sawa na asilimia 2, kati yao wanawake1,181 na wanaume ni 703.
Akibainisha ratiba ya wiki ya maadhimisho hayo Mhe. Adama Malima amesema Maadhimisho hayo yanaenda sambamba na kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, yenye ujumbe usemao “Wekeza kuzuia ukatili wa kijinsia”. Kampeni hiyo itahitimishwa tarehe 10 Disemba, 2023.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) Dkt. Jerome Kamwela amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano aliutoa hadi kufanikisha maadhimisho hayo.
Naye mwakilishi wa Baraza la watu waishio na VVU (NACOPHA) Bw. Emanuel Msinga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma mbalimbali zikiwemo za Afya na kutoa fursa kwa wananchi waishio na VVU kupata mikopo ambayo imewasaidia kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.