Mwili wa aliyekuwa mke wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro waagwa, Waziri Ummy aongoza shughuli ya kuuaga.
Mwili wa aliyekuwa mke wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bi. Magdalena Layda Shigela umeagwa leo Jan. 22, 2022 huku viongozi mbalimbali wa chama na Serikali pamoja na waombolezaji wakishiriki kuuga tayari kwa safarishwa kwenda Kishapu Mkoani Shinyanga kwa maziko.
Shughuli ya kuaga mwili wa marehemu Magdalena imeongozwa na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu (Mbunge) nyumbani kwa marehemu Salasala, Mtaa wa Kilimahewa Jijini Dar es Salaam akishirikiana na viongozi wengine wa chama na Serikali akiwemo Waziri wa Madini Dotto Biteko na Katibu wa Chama cha Mapinduzi Taifa Daniel Chongolo pamoja na Naibu wake Cristine Mndeme.
Akiwasilisha salamu za Serikali, Waziri Mwalimu ametoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela kwa kuondokewa na Mpendwa wake na kwamba kwa niaba ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na viongozi wengine wa serikali anatoa pole na wako pamoja katika kipindi hiki kigumu.
“Naomba pia upokee salamu zao za pole kwa niaba yao, hatuna mengi ya kusema kwa sababu hayo ni matakwa ya mwenyezi Mungu” amesema Waziri Ummy.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi, Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Bi. Christine Mndeme pamoja na kuwataka waombolezaji kumuombea marehemu Magdalena, amewataka pia ndugu, jamaa, marafiki na waombolezaji waliofika kwenye msiba huo kuyaenzi yote mazuri aliyoyafanya Magdalena enzi za uhai wake.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martine Shigela akiwa na watoto wake Lorenzo na Loveness wakati wa kuaga mwili wa mke wake Bi.Magdalena Layda Shigela.
Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa wote Tanzania Bara, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Wilbert Ibuge amesema wakuu wa Mikoa wanatambua uzito alionao Martin Shigela pamoja na familia yote kwa kuondokewa na Mpendwa wao na kwamba kazi nyingi za Kiserikali alizofanikiwa kuzifanya shigela zinatokana na maisha ya Amani, utulivu na Upendo uliokuwa umetawala katika familia yao, hivyo anahitaji kuombewa zaidi kustahimili kipindi kigumu anachopitia.
Wakiwasilisha salamu za Mkoa wa Morogoro, Mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi Mkoa wa Morogoro Mhe. Dorothy John amemtaka Kiongozi wao Mhe. Martine Shigela kumtegemea mungu katika kipindi anachopitia, huku Katibu Tawala wa Mkoa huo Bi. Mariam Mtunguja kwa ya watumishi wote wa Serikali Mkoa wa Morogoro ametoa pole nyingi kwa Mhe. Martine Shigela na familia nzima na kuwatakia utulivu wa moyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro martine Shigela pamoja na kuwashukuru watu mbalimbali kwa namna ambavyo wamejaribu kuokoa maisha ya mkewe bila mafanikio na namna walivyomkimbilia wakati wa msiba amesema msiba huo kwake ni mzito na unapelekea kuanza upya maisha mengine kwa uzito wake.
“msiba huu kwangu ni mzito sio mdogo, naanza maisha ambayo sikuwahi kuyapitia ……niombeeni, maisha magumu sana“ amesisitiza Martine Shigela.
Marehemu Magdalena Layda alizaliwa mwaka 1975, amefariki usiku wa kuamkia Januari 20 mwaka huu, ameacha watoto wawili ambao ni Lorenzo na Loveness na anatarajiwa kuzikwa Kishapu Mkoani Shinyanga Januari 24 mwaka huu.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina la Bwana lihimidiwe. Amina.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.